
IKULU
ya Rais wa Marekani imeyazuia mashirika kadhaa makuu ya habari nchini
humo kuhudhuria kikao cha wanahabari kilichoendeshwa na msemaji wa
Ikulu, Sean Spicer.
Wanahabari wa
Mashirika ya CNN, The New York Times, Politico, Los Angeles Times na
BuzzFeed hawakuruhusiwa kuhudhuria kikao cha wanahabari katika ofisi ya
Msemaji wa Ikulu ya Rais wa Marekani.
Wamelaani
kitendo hicho na kukiita kuwa ni cha kibaguzi dhidi ya vyombo vya
habari na wanahabari wenyewe. Utawala wa Rais Donald Trump umekuwa
ukiyashutumu mashirika hayo kuwa yanaeneza habari za uongo na za
kupotosha.
Spicer hakutoa maelezo;
kwanini waandishi wa habari wa mashirika hayo waliachwa nje ya kikao
kisicho rasmi cha wanahabari, hatua ambayo imeibua shutuma kali.
Shirika
la Habari la Reuters pamoja na mashirika mengine 10 yakiwemo Bloomberg
na CBS yaliruhusiwa kuhudhuria mkutano huo wa wanahabari.
Wakati
wanahabari kutoka CNN na mashirika mengine yaliyoathiriwa yalipojaribu
kuingia IKulu, yalizuiwa kwa kuambiwa majina yao hayako katika orodha ya
wanahabari walioalikwa.
Katika
mkutano wa wanaharakati wa kisiasa wa Jumuiya ya CPAC juzi, Rais Trump
alivishutumu baadhi ya vyombo vya habari ambavyo anadai vinatoa taarifa
za uongo na kuvitaja kuwa adui ya watu wa Marekani.
Spicer
alisema kundi lake liliamua kufanya mkutano mdogo wa wanahabari katika
ofisi yake badala ya mkutano rasmi wa wanahabari kama ilivyo desturi
katika chumba cha wanahabari katika Ikulu ya Rais akihoji hawahitaji
kuendesha kila kitu mbele ya kamera kila siku.
Wanahabari
kutoka mashirika ya Associated Press na Jarida la Time waliondoka
kutoka kwenye kikao hicho walipoarifiwa kuwa wanahabari wenzao kutoka
mashirika mengine wamezuiwa kuhudhuria kikao hicho.
Taarifa
kutoka kwa Mhariri Mkuu wa The New York Times; Dean Baquet ilisema
jambo kama hilo halijawahi kutokea katika Ikulu ya Rais ya White House
katika historia yao ndefu ya kuripoti taarifa kutoka tawala chungu nzima
kutoka vyama tofauti vya kisiasa nchini Marekani.
Baquet
alisema wanapinga kuzuiwa kwa gazeti lao na mashirika mengine ya habari
na kuongeza kuruhusiwa kwa vyombo hivyo kuwa na uhuru na kuangazia
matukio ya serikali iliyo wazi bila shaka ni muhimu kwa maslahi ya
taifa.
Chama cha maripota wa Ikulu ya White House (WHCA) pia kimepinga hatua hiyo ya Spicer.
Rais
wa chama hicho, Jeff Mason ambaye ni ripota wa Reuters alisema
wanapinga jinsi kikao hicho kilivyoendeshwa na Ikulu ya White House.
Katika
kipindi cha kampeni mwaka jana, kundi la Trump liliyapiga marufuku
mashirika kadhaa likiwemo gazeti la Washington Post na Buzzfeed dhidi ya
kuripoti katika mikutano ya kampeni likiyashutumu kwa upotoshaji na
kueneza habari za uongo
No comments:
Write comments