
Wakala
wa Barabara Tanzania (Tanroads), umetiliana saini ya ujenzi wa daraja
la Ubungo na Kampuni ya China Civil Engeneering Constraction Corporation
(CCECC), ambao unatarajiwa kuanza mwezi ujao na kugharimu zaidi ya Sh.
bilioni 177.
Utiaji saini huo unakuja
siku chache baada ya Rais John Magufuli kumuomba Makamu wa Rais wa Benki
ya Dunia (WB) upande wa Afrika, Makhtar Diop kusaidia ujenzi huo wakati
wa uzinduzi wa usafiri wa mabasi ya mwendokasi.
Mtendaji
Mkuu wa Tanroads, Mhandisi Patrick Mfugale alibainisha hayo
alipozungumza na waandishi wa habari jana baada ya utiaji saini
makubaliano hayo makao makuu ya wakala huo jijini Dar es Salaam, huku
ikibainishwa jengo la Makao makuu ya Tanesco halitaguswa na ujenzi wa
daraja hilo la ghorofa tatu.
Mfugale
alisema makubaliano yao ni kuwa ujenzi uanze kuanzia sasa na utadumu kwa
miezi 30 ili kuondoa changamoto ya foleni kwenye eneo la Ubungo.
Alisema
WB imetoa mkopo huo ambapo mkandarasi atalipwa moja kwa moja na Sh.
bilioni 8.2 atalipwa mhandisi mshauri kwa ajili ya usimamizi ambaye ni
Kampuni ya M/s Dasan ya Korea Kusini ikishirikiana na Kampuni ya Afrika
Ltd ya Tanzania.
“Tumetiliana saini
ujenzi wa Daraja la Ubungo ‘interchange’ na Kamapuni ya CCECC ambapo
zaidi ya Sh.bilioni 177 zitatumika na litakuwa daraja la ghorofa tatu ni
kazi ya miezi 30,” alisema.
Mfugale
alisema safu ya chini ya daraja hilo itatumika kwa magari ya Barabara ya
Morogoro na kupinda kushoto na safu ya pili itajengwa katika urefu wa
mita 5.75 kutoka usawa wa ardhi na itatumika kwa magari yote yanayopinda
kulia na kuongozwa taa za barabarani.
Alisema
Safu ya tatu itajengwa kwa urefu wa meta 11.5 kutoka usawa wa ardhi na
itatumika kwa magari yanayopita Barabara za Mandela na Sam Nujoma na
barabara zote zitakuwa na njia sita.
Mtendaji
huyo alisema kampuni 48 ziliomba zabuni ila ni 14 ambazo zilirejesha
hivyo baada ya kupitia kwa makini CCECC ilifanikiwa kushinda.
Alisema
upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ulifanywa na Kampuni ya M/s Hamza
Associates ya Misri kwa kushirikiana na Kampuni ya Advanced Engineering
Solutions Ltd ya Tanzania kwa gharama ya zaidi ya sh. milioni 951 ambapo
kazi ilikamilika Desemba 2016
No comments:
Write comments