Thursday, 16 March 2017

Makamu wa Rais Samia Suluhu amewasili mjini Mbabane – Swaziland leo kuhudhuria mkutano wa Wakuu wa nchi


Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amewasili mjini Mbabane – Swaziland leo kwa ajili ya kuhudhuria mkutano wa Wakuu wa nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mfalme Mswati III mjini Mbabane ñ Swaziland, Makamu wa Rais amepokelewa na Viongozi mbalimbali ambao wameongozwa na Waziri wa Utumishi wa Umma wa Serikali ya Swaziland Owen Nxumalo.

Makamu wa Rais atamuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania Dakta JOHN POMBE MAGUFULI ambaye pia ni Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama inayojulikana kama SADC DOUBLE TROIKA kwenye mkutano huo.

Kesho Makamu wa Rais atahudhuria mkutano wa Wakuu na Serikali wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama unaojulikana kama SADC Double Troika ambao utajadili kwa kina hali ya ulinzi na usalama katika nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC)na Falme ya Lesotho.

Mkutano huo wa SADC Double Troika utafanyika kwa kuzingatia mapendekezo ya mkutano wa Mawaziri wa Kamati Ndogo ya Siasa na Diplomasia uliofanyika Dar es Salaam februari 24 mwaka huu ambapo mawaziri hao walionyesha ipo haja ya kuitisha mkutano huo ili kujadili kwa kina hali ya ulinzi na usalama.

Mkutano wa SADC Double Troika utahusisha nchi Sita wanachama wa asasi hiyo ambazo ni Tanzania, Swaziland, Afrika Kusini, Angola, Botswana na Msumbiji.

No comments:
Write comments