RAIS wa Benki ya Dunia (WB), Dk Jim
Yong Kim anatarajiwa kuwasili nchini keshokutwa na Jumatatu ijayo akiwa
na Rais John Magufuli, wataweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya
juu (mzunguko) eneo la Ubungo, Dar es Salaam ambayo itasaidia kupunguza
msongamano wa magari jijini humo.
Kwa mujibu wa taarifa ya Benki ya Dunia,
atafanya ziara ya siku tatu nchini kuanzia keshokutwa na Dk Kim
atakutana na Rais Magufuli na kufanya naye mazungumzo muhimu ya
kuimarisha ushirikiano wa kimkakati baina ya Tanzania na benki hiyo na
pia kutembelea miradi ya uwekezaji inayofadhiliwa na benki yake katika
miundombinu na kusisitizia haja ya kuendelea kuunga mkono uwekezaji
katika maendeleo ya jamii hususani ubora wa elimu na kuwekeza katika
elimu ya awali.
Dk Jim akiwa na mwenyeji wake Rais
Magufuli ataweka jiwe la msingi la ujenzi wa njia ya makutano eneo la
Ubungo na pia atatembelea Shule ya Msingi Zanaki iliyopo Upanga.
Hii ni mara ya kwanza kwa Rais huyo wa Benki ya Dunia kutembelea Tanzania.
Benki ya Dunia hivi sasa inafadhili jumla
ya miradi 23 ya kitaifa nchini yenye thamani ya dola za Marekani bilioni
3.6, na sehemu kubwa ya miradi hiyo inahusika na ujenzi wa miundombinu
ya usafiri na miradi ya maendeleo vijijini
No comments:
Write comments