RAIS
John Magufuli ameagiza kwamba, ikifika Jumatano wiki ijayo, mazungumzo
kati ya Wizara ya Nishati na Madini na bilionea Aliko Dangote yawe
yamekwisha ili gesi ipatikane kwenye kiwanda cha saruji cha
mfanyabiashara huyo.
Ameagiza kwamba, Wizara hiyo ijadiliane na Dangote mwenyewe badala ya kupitia kwa watu aliowaita kuwa ni matapeli.
Ametoa maagizo hayo leo kabla ya kuzindua magari 580 ya Dangote yatakayotumika kusambaza saruji kutoka kiwandani hapo.
Amewatuhumu
baadhi ya wawakilishi wa mfanyabiashara huyo kuwa wanachelewesha
uwekezaji na huenda wanashirikiana na viwanda vingine vya saruji
kuihujumu Serikali.
“Inawezekana watu
wako wanaokuwakilisha wana matatizo, hii ni meseji kwa mheshimiwa
Dangote mwenyewe, ni lazima awe mwangalifu kwa watu wake”amesema Rais
Magufuli.
Amesema, mfanyabiashara huyo
ni mwekezaji muhimu sana Tanzania kwa kuwa amewezesha maelfu ya
Watanzania kupata ajira na pia Serikali inapata mapato kupitia kodi.
Amemshukuru
Dangote kwa kuwekeza Tanzania na pia amemshukuru Rais wa Awamu ya Nne,
Jakaya Kikwete kwa kusimamia mchakato uliowezesha kujengwa kwa kiwanda
kikubwa cha saruji mkoani Mtwara.
“Mheshimiwa Kikwete popote ulipo asante sana na Mungu akubariki” amesema Rais Magufuli
No comments:
Write comments