Wafanyabiashara
sita wamekufa papo hapo na wengine 12 kujeruhiwa, baada ya lori
lililokuwa likiwapeleka mnadani kuacha njia na kuporomoka kwenye mlima
wenye kona nyingi zinazofikia 99 wilayaniLushoto.
Taarifa
zilizopatikana na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga,
Benedict Wakulyamba zilisema ajali hiyo ilitokea jana Jumapili jioni
katika mlima wenye idadi hizo za kona zinazoanzia Mng’aro hadi Mlalo
wilayani Lushoto, baada ya lori aina ya Mitsubishi Fuso Canter
kuporomoka.
Watu
walioshuhudia ajali hiyo walisema lori hilo lilikuwa likitokea Kijiji
cha Mng’aro kilichopo uwanda wa chini lilipokuwa likipanda mlima
kuelekea Mlalo kwa ajili ya kuwahi soko siku inayofuata.
Walisema
lori hilo lilipofika katikati ya mlima liliacha njia na kurudi nyuma
hatimaye likaporomoka bondeni, huku mizigo ikiwaangukia watu hao.
Kamanda
Wakulyamba aliwataja waliokufa kuwa ni Jamal Hemed (40), mkazi wa
Mlalo, Hassan Rashid (33) wa Nyasa, Bisura Seif wa Kifungilo, Hadija
Said wa Mhelo, Zuena Juma wa Kwedege na Husna Athumani wa Hemtoye.
Alisema
majeruhi wa ajali hiyo walipelekwa katika Hospitali ya Wilaya ya
Lushoto kwa matibabu. Kamanda huyo alisema dereva wa lori hilo, Nassoro
Athumani (25) anatafutwa kwa kuwa alitoroka baada ya ajali.
No comments:
Write comments