RUFAA ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali dhidi ya Mbunge wa Arusha Mjini,
Godbless Lema (Chadema) inatarajiwa kusikilizwa leo katika Mahakama Kuu
Kanda ya Arusha.
Rufaa hiyo itasikilizwa na jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani
ambao ni Stella Mugasha, Kipenka Mussa na Bernard Luanda ambaye atakuwa
mwenyekiti.
Kesi ya Lema ilikwama kutolewa uamuzi na Jaji Salma Magimbi, Januari 4,
mwaka huu, baada ya Wakili wa Serikali, Innocent Njau, kuiomba mahakama
hiyo kutoendelea na kesi hiyo kwa sababu wamekata Rufaa Mahakama ya
Rufani, kupinga Jaji Dk. Modesta Opiyo, kumwongezea Lema muda wa siku 10
ili akate rufaa ya kunyimwa dhamana, nje ya muda.
Pia katika rufaa hiyo, itasikilizwa kesi ya mawakili wa Lema wanaopinga
Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha kukubali kumpa dhamana Lema.
Awali Jaji Salma Magimbi, alisema kwa kuwa upande wa Jamuhuri umekata
rufaa hataweza kuendelea kutoa uamuzi wa rufaa ya Lema kulalamikia
kunyimwa dhamana katika Mahakama ya Hakimu mkazi Arusha.
Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha ilimpa dhamana Lema lakini kabla ya
kusomewa masharti yake, mawakili wa Jamuhuri waliwasilisha kusudio la
mdomo la kukata rufaa Mahakama Kuu kupinga uamuzi wa hakimu.
Jaji Dk. Opiyo alitoa uamuzi Desemba 20 mwaka jana wa kumwongezea Lema
muda wa siku 10, ili akate rufaa ya kupinga kupewa dhamana bila masharti
ya dhamana, na kutupa pingamizi mbili za wanasheria wa serikali,
waliopinga kusikilizwa kwa rufaa hiyo kwa sababu ipo nje ya muda
kisheria.
Jaji Dk. Opiyo alisema hoja hizo hazikuwa na mashiko.
Lema alianza kukaa mahabusu Novemba 2, mwaka jana, baada ya kukamatwa
katika viwanja vya Bunge mjini Dodoma na kusafirishwa kuletwa Kituo
Kikuu cha Polisi Mkoa wa Arusha.
Novemba 8 alifikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha mbele ya Hakimu
Desderi Kamugisha ambapo alisomewa shitaka la uchochezi dhidi ya Rais
John Magufuli.
Hakimu Kamugisha alikubali kutoa dhamana kwa Lema kwa madai kuwa sheria
haizuii kutoa haki hiyo kwa mshtakiwa wa kesi ya uchochezi lakini kabla
ya kutamka masharti ya dhamana, Mawakili wa Serikali, Paul Kadushi na
Materius Marandu walidai wana nia kukata rufaa dhidi ya msimamo huo.
Kutokana na mawakili hao kusema hivyo, Hakimu aliamua kesi hiyo ibaki
kama ilivyo, huku mtuhumiwa akisubiri maamuzi ya rufani ya Jamhuri
katika Mahakama Kuu.
Jaji Dk. Opiyo alipotupa rufaa ya Jamhuri na kumpa Lema siku 10 zaidi
ili akate rufaa ya kupinga kupewa dhamana bila masharti ya dhamana kwa
kuwa hoja hizo hazikuwa na mashiko, mawakili wa serikali wakakata rufani
Mahakama ya Rufani.
No comments:
Write comments