Sunday, 19 March 2017

Dk Shein: Hakuna wakuniondoa madarakani


Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein ametua kisiwani Pemba na kuwataka wananchi kufanya kazi, huku akisisitiza hakuna atakayemuondoa madarakani.

Dk Shein amesema hayo ikiwa takriban siku 30 tangu Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad afike na kuzungumza na wananchi akiwahakikishia kuwa, ‘haki yao wataipata hivi karibuni’.

Rais Shein ametoa kauli hiyo akiwa katika Sekondari ya Fidel Castro iliyopo Mkoa wa Kusini Pemba alikokwenda kwa ajili ya kugawa vifaa vya michezo kwa maandalizi ya ligi ya mpira wa miguu kwa timu 18 za kisiwani humo.

Timu hizo zitashindana kusherehekea mwaka mmoja tangu alipoapishwa kuwa Rais wa Zanzibar katika awamu ya pili na kusherehekea miaka 40 ya kuzaliwa kwa CCM.

Dk Shein amewataka wananchi kuepuka maneno ya kizushi kuwa kuna Serikali itakuja kuiondoa madarakani anayoiongoza.

Amesema katika siku za karibuni hakutakuwa na uchaguzi mwingine mpaka mwaka 2020 ambao pia chama anachokiongoza anaamini kitashinda na kuendelea kushika dola.

Katika ziara hiyo pia ameambatana na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Abdalla Juma Abdalla ‘Mabodi’ aliyetumia fursa huyo kutoa shukrani kwa kuteuliwa kushika wadhifa huo mjini Dodoma hivi karibuni

No comments:
Write comments