Friday, 24 March 2017


Korea Kaskazini: Nani alimrukia Kim Jong-un?

Korea Kaskazini ilipokuwa inafanyia majaribio injini mpya ya kurusha roketi na makombora, tukio hilo liliangaziwa na vyombo vya habari vya taifa hilo kama ilivyo kawaida.

Lakini kuna picha moja iliyovutia na kushangaza zaidi.
Ni picha ya mwanamume aliyeruka na kuonekana kana kwamba anabebwa na kiongozi huyo alipokuwa anasherehekea ufanisi wa majaribio hayo..

Kim Jong-un bila shaka alionekana kuwa mwenye furaha isiyo na kifani.
Lakini mbona mtu amrukie mgongoni kiongozi wa kiimla, na ni nani anaweza kuthubutu kufanya hivyo?

Wachanganuzi wanasema mwanamume huyo hana umaarufu mkubwa katika siasa za Korea Kaskazini.

Hata hivyo, inadhaniwa huenda alitekeleza mchango muhimu katika majaribio hayo ya injini, na kuna uwezekano mkubwa huenda aliwahi kukutana na kujumuika na Kim awali.

Mchanganuzi wa masuala wa Korea Kaskazini Michael Madden anasema nembo za cheo kwenye sare yake zinaashiria kwamba ni afisa wa ngazi wa wastani katika kikosi cha Wanajeshi Maalum wa Angani wa Korea Kaskazini.

Kikosi hicho ndicho husimamia makombora yanayotumiwa kutekeleza mashambulio nchini humo.
Ingawa kuna uwezekano kwamba huenda picha hiyo iliigizwa, Bw Madden, anayefanya kazi katika Taasisi kuhusu Korea Kusini katika Chuo Kikuu cha Johns Hopkins, anasema baadhi ya yaliyojitokeza "si ya kuigizwa kabisa".

"Zaidi ilikuwa kama ishara ya kutoa nafasi (na kuwakubali wengine) pamoja na kuwapa moyo badala ya kuwa sana picha iliyoigizwa."

Filamu za propaganda za Korea Kaskazini awali zimewahi kuwaonesha raia wakiruhusiwa kumkaribia Kim.

'Rafiki na mcheshi'
Lengo kuu la kutoa picha hiyo huenda lilikuwa kuendeleza sifa za Kim nchini mwake kama mtu mwenye furaha na anayewapenda watu wake.

Ingawa Kim hujaribu kujionesha kuwa mtu mwenye msimamo mkali kimataifa, nyumbani hali ni tofauti kwa mujibu wa Profesa Jae-Cheon Lim, wa Chuo Kikuu cha Korea mjini Seoul.

"Tunajua kwamba yeye huwa mkali sana kwa maafisa wa serikali na wasomi wanapokiuka amri zake. Lakini kwa jumla, kwa raia, hujionesha kama rafiki na mcheshi."

KIm anaonekana kuwa tofauti sana na watangulizi wake, ambao walitaka zaidi kuogopwa badala ya kupendwa na wananchi.

"Hakuna mtu angethubutu kumrukia baba yake au hata babu yake mgongoni," anasema Bw Madden.
"Lakini hili linaendana sambamba na picha na sifa ambazo Jong-un amejaribu kujizolea - kwamba yeye ana uwazi zaidi na huwakaribisha watu, kuliko baba yake.

"Ni jambo linaloashiria hisia fulani za kujiamini kisiasa kuhusu utawala wake na uongozi wake nchini humo.

Kama hangejihisi kuwa salama, basi hangeruhusu picha hizi zisambazwe - angetaka kuonekana zaidi kama mtu aliye mbali na watu na asiyewakaribisha watu kwake."

Picha hiyo, pia, inajaribu kuonesha kwamba Kim yuko na afya nzuri.
Alionekana akichechemea na kutumia mkongojo mwaka 2014, jambo lililozua uvumi kwamba huenda alikuwa anaugua ugonjwa wa jongo.

Alionekana akichechemea tena majuzi mwaka 2016.
Wachezaji soka

Tabia ya kuwarukia watu wengine migongoni na kubebwa sana huonekana katika viwanja vya soka.
Lakini Kim anajulikana kuwa mtu anayechukua mtazamo wa usimamizi wa soka katika miradi yake ya kustawisha silaha.

"Jaribio linapotekelezwa, raia na wanajeshi (huambiwa) kwamba wanafaa kulichukulia kama shindano michezoni - wanashinda baadhi, na kushindwa baadhi ya mashindano," anasema Bi Madden.

"Hawatashinda au kutimiza mahitaji yote ya kiufundi wakati wote, na wanaposhindwa wanahitaji kutathmini utendaji wao na yale yaliyotendeka."

Lakini haya hayana maana kwamba Kim hakuwa na furaha kwenye picha hiyo.
Prof Lim anasema alikuwa na sababu tosha ya kufurahi - kwamba jaribio la injini ya kurusha roketi lilifanikiwa na kumsaidia kupiga hatua katika kukaribia kutimiza malengo yake ya kustawisha silaha za nyuklia

No comments:
Write comments