Lissu Afunguka Mazito Juu ya Rais Magufuli Kutoteua Jaji Mkuu Hadi Sasa
HATUA
ya Rais John Magufuli kumteua Profesa Ibrahim Juma kuwa Kaimu Jaji Mkuu
wa Tanzania imeibua utata kuhusu dhamira yake kwenye kufanya hivyo,
Raia Mwema limeambiwa.
Tangu Uhuru wa Tanganyika, hakuna Rais
aliyewahi kumteua mtu kuwa Kaimu Jaji Mkuu; baada ya Jaji Mkuu
aliyekuwepo madarakani kumaliza muda wake wa utumishi kwenye mhimili huo
wa dola.
Profesa Juma ambaye anachukuliwa kama
mgeni kwenye mhimili huo, aliteuliwa na Rais Magufuli mapema mwaka huu
kuwa Kaimu Jaji Mkuu akichukuwa nafasi ya Chande Othman aliyefikia umri
wa kustaafu.
Mazungumzo baina ya gazeti hili na
wandani wa Mahakama hapa nchini yameeleza hali hiyo kuleta utata kwa
vile tukio hilo halijawahi kutokea na halina maelezo ya maana kulitetea.
“Sikiliza, hii nchi haijawahi kuwa na
Kaimu Jaji Mkuu aliyeapishwa wakati Jaji Mkuu akiwa amestaafu. Hii ni
mara ya kwanza na kwa kweli imeleta mkanganyiko mkubwa.
“ Kaimu Jaji Mkuu anaweza kuapishwa
wakati Jaji Mkuu akiwa kwenye safari ya muda mrefu nje ya nchi au akiwa
na tatizo linaloweza kuathiri utendaji kazi wake. Hapo Kaimu anaweza
kuapishwa lakini si kwa ilivyo sasa. Jaji Mkuu kastaafu sasa Rais
anateua Kaimu wa nini?” alihoji mmoja wa majaji mashuhuri nchini
aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa majina yake.
Jaji huyo alisema mtu akiwa anakaimu
nafasi yoyote anakuwa hajiamini na hawezi kuchukua uamuzi mzito kwa
sababu hajui kama atamfurahisha aliyemteua au la.
“Kama Rais alikuwa anamtaka Profesa Juma,
angemteua tu kuwa Jaji Mkuu, hii kaimu haina maana sana. Imeleta
mkanganyiko na utata tu,” alisema Jaji huyo.
Ingawa baadhi ya wanaharakati kwenye
baadhi ya mitandao ya kijamii wameenda mbali kiasi cha kusema kuna
uvunjwaji wa Katiba kwenye uteuzi huo wa Kaimu Jaji Mkuu, Raia Mwema
limebaini hakuna uvunjwaji wa Katiba uliofanyika kwenye jambo hilo.
Ibara ya 118 ya Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania toleo la mwaka 197, imeeleza kwa kirefu kuhusu
nafasi hiyo ya Jaji Mkuu kama ifuatavyo:-
“118.-(1) Kutakuwa na Jaji Mkuu wa Mahakama ya Rufani
(ambaye katika ibara zifuatazo kwenye
Katiba hii atatajwa tu kwa kifupi kama “Jaji Mkuu” na Majaji wengine wa
Mahakama ya Rufani wasiopungua wawili, isipokuwa kwamba kikao maalumu
cha Mahakama nzima kitakuwa kamili kikiwa na Majaji wa Rufani
wasiopungua watano.
(2) Jaji Mkuu atateuliwa na Rais na
atakuwa ndiye Kiongozi wa Mahakama ya Rufani na pia Mkuu wa Idara ya
Mahakama kama ilivyofafanuliwa katika ibara ya 116 ya Katiba hii.
“(3) Majaji wengineo wa Mahakama ya
Rufani watateuliwa na Rais, baada ya kushauriana na Jaji Mkuu, kutoka
miongoni mwa watu ambao wanaweza kuteuliwa kuwa Majaji wa Mahakama Kuu
ya Jamhuri ya Muungano kama ilivyoelezwa katika ibara ya 109 ya Katiba
hii au kutoka miongoni mwa watu wanaoweza kuteuliwa
kuwa Majaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar kwa mujibu wa Sheria zinazotumika Zanzibar.
“(4) Iwapo itatokea kwamba:-
(a) Kiti cha Jaji Mkuu kitakuwa wazi; au
(b) Jaji Mkuu hayupo Tanzania; au
(c) Jaji Mkuu atashindwa kutekeleza kazi
yake kwasababu yoyote na Rais akiona kuwa kwa muda watukio lolote kati
ya hayo matatu inafaa kumteua Kaimu Jaji Mkuu, basi Rais aweza kumteua
Kaimu Jaji Mkuu kutoka miongoni mwa watu wenye sifa za kustahili
kuteuliwa kuwa Majaji wa Mhakama ya Rufani.
“Na huyo huyo Kaimu Jaji Mkuu atatekeleza
kazi za Jaji Mkuu mpaka atakapoteuliwa Jaji Mkuu au mpaka Jaji Mkuu
mwingine ambaye hakuwapo Tanzania au alikuwa hamudu kazi zake
atakaporejea kazini.”
Kwa mujibu wa vifungu hivyo vya Katiba,
Rais anaweza kuteua Kaimu Jaji Mkuu endapo “Kiti cha Jaji Mkuu kitakuwa
wazi”; lakini haijafafanua uwazi upi kwani inaweza kuwa kwa sababu ya
kifo, kustaafu, kusafiri, kuumwa au sababu nyingine yoyote
inayokubalika.
Ukaimu wa Profesa Juma
Baadhi ya wandani hao wa Mahakama,
wameliambia gazeti hili ingawa imekuwa ni kawaida kwa majaji kukaimu
Ujaji Mkuu, mara nyingi wanaokaimu huendelea kutumia ofisi zao zilezile
na magari yaleyale, jambo ambalo ni tofauti na sasa.
Raia Mwema limeelezwa kwamba Profesa Juma
anatumia gari la Jaji Mkuu, anafanya kazi kwenye ofisi ya Jaji Mkuu na
kutendewa kama Jaji Mkuu kamili, ilhali wadhifa wake huo
haujathibitishwa.
Wakati wa Jaji Mkuu Francis Nyalali, Raia
Mwema limeelezwa, mara kadhaa aliwahi kutibiwa nje ya nchi na nafasi
yake kukaimiwa na Jaji Augustino Ramadhani, lakini hakuwahi kutumia gari
wala ofisi ya Jaji Mkuu.
Ilikuwa hivyo hivyo kwa Jaji Eusebia
Munuo ambaye aliwahi kukaimu nafasi ya Chande wakati alipokuwa nje ya
nchi kwa muda mrefu lakini hakuwahi kutumia ofisi ya Jaji Mkuu wala gari
lake.
“ Kwa mujibu wa Sheria za Utumishi, muda
wa kukaimu nafasi ni miezi sita. Sasa tunasubiri kwa hamu baada ya
kupita kwa miezi hiyo sita nini kitafuata.
“ Je, Rais Magufuli atamuita tena Jaji
Juma kwa ajili ya kumuapisha kuwa Jaji Mkuu? Kama hatamuapisha, atatoa
sababu za kutomuapisha? Je, watu wakisema amemtoa kwa sababu alikataa
kuburuzwa itakuwaje?” Raia Mwema limeambiwa.
Akizungumza na gazeti hili kuhusu suala
hili, Rais wa Chama cha Mawakili wa Tanganyika (TLS), Tundu Lissu,
alisema hatua ya Rais Magufuli kuteua Kaimu Jaji Mkuu ni dharau kubwa
kwa majaji wa Tanzania.
Alisema kitendo cha Rais kuteua Kaimu
Jaji Mkuu wakati kulikuwa na fursa ya kuteua Jaji Mkuu kamili kinatoa
picha mbili kubwa; moja kwamba hakuwa tayari kwa uteuzi huo na pili
hakuna majaji wenye sifa ya kuchukua wadhifa huo.
“Je, Rais anataka kuonyesha kwamba nchi
hii haina majaji wenye uwezo wa kushika wadhifa huo kiasi kwamba ateue
Kaimu Jaji Mkuu? Kwangu, naichukulia hii kuwa ni dharau kwa majaji wetu.
“ Mimi nasema Rais hajavunja sheria
yoyote kwa kuteua Kaimu Jaji Mkuu lakini kinachogomba hapa ni picha
anayoionyesha kwa mhimili huu. Kinachogomba ni dhamiri yake kwenye Idara
ya Mahakama,” alisema Lissu.
Lissu alisema kazi iliyopo sasa kwa
wanasheria, asasi za kijamii na vyombo vya habari ni kumkumbusha Rais
kwa nguvu zote kwamba Idara ya Mahakama inatakiwa kuongozwa na Jaji Mkuu
mwenye mamlaka kamili na si ya kukaimu.
“Na nyie mjiulize, Jaji Mkuu amestaafu,
Kaimu Jaji Mkuu wa nini? Kaimu inakubalika tu wakati mhusika anapokuwa
nje ya nchi au kwa sababu nyingine kama zilivyoelezwa kwenye Katiba.
Hili la kuteua Kaimu wakati Jaji Mkuu amestaafu ndiyo kalileta
Magufuli,” alisema.
Jaji Ibrahim Hamis Juma ni msomi mbobezi
wa masuala ya sheria akiwa amewahi kuwa Mkuu wa Kitivo cha Sheria cha
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Aliapishwa kuwa Kaimu Jaji Mkuu Januari mwaka huu na kwa mara ya kwanza aliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu mwaka 2008.
Credit – Raia Mwema
No comments:
Write comments