MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul
Makonda, ameadhimisha mwaka mmoja wa kuwa kwenye kiti hicho kwa kula
chakula cha mchana na waathirika wa dawa za kulevya, huku akizungumzia
mafanikio aliyopata katika uongozi wake.
Licha ya kueleza mafanikio aliyopata,
hakugusia kuhusu tuhuma mbalimbali zilizoelekezwa kwake na watu
mbalimbali, badala yake alisema hakuna wa kumtisha wala kumnyamazisha na
kwamba sasa ndiyo amepata nguvu mpya baada ya kupata mashambulizi
mbalimbali.
Pia mkutano huo uliofanyika katika Ukumbi
wa Maofisa wa Polisi, Oysterbay, Dar es Salaam, ulihudhuriwa na watu
wachache wakiwamo waandishi kutoka vyombo vichache vya habari, tofauti
na mikutano yake mingine ambayo alikuwa akialika vyombo vingi vya
habari.
“Mwaka wangu wa pili katika uongozi ambao
unaanza , speed (kasi) ya hali ya utumishi wangu itaongezeka mara mbili
zaidi kwa sababu nimeshakomaa, lazima Dar es Salaam iwe kwenye mazingira
salama.
“Eti mtu anataka nikae kimya wakati
wananchi wangu wa Dar es Salaam wanateseka kwa matumizi ya dawa za
kulevya… nauliza wewe ni nani uninyamazishe na umetoka wapi?” alihoji
Makonda.
Alisema pamoja na changamoto nyingi
anazopitia, hajawahi kutetereka wala kutingishwa na kwamba yuko tayari
idadi ya wanaomchukia iongezeke kwa sababu hahitaji kupendwa.
“Sijawahi kutetereka wala sijawahi
kutingishwa. Kazi hii nimepewa na Mungu, acha idadi ya wanaonichukia
iongezeke kwa sababu sihitaji kupendwa, lakini niwe na uhakika na Mungu
wangu.
“Mara nyingi ninapochapwa na mawimbi makali, mke wangu amekuwa akizama kwenye sala na kuniombea,” alisema.
Alisema anafanya kazi hiyo kwa upendo na kwamba hana kisasi na yeyote.
“Tunayafanya haya kwa upendo, hatuna
kisasi na yeyote, ndiyo maana sisi tunafurahi, lakini upande wa pili
wanapambana, kazi yetu ni kumulika watu,” alisema Makonda.
Aidha alisema wameamua kupigana vita ya dawa za kulevya hadharani kwa sababu hataki kupokea rushwa wala fedha haramu.
Makonda alisema kupitia fedha za dawa za
kulevya, wengi wamejenga maghorofa na wamesababisha hata bei ya viwanja
ipande, hivyo atahakikisha fedha hizo zinakauka ili kila mtu ale kwa
jasho lake.
Alisema lengo lake ni kupambana kupigania
ndoto za vijana na matumaini ya wazazi wao na haijalishi kama
amechelewa, lakini hataacha.
Makonda alisema hababaishwi na watu
wanaomchukia wakati akitekeleza majukumu aliyopewa na Rais Dk. John
Magufuli kama Mkuu wa Mkoa.
Alisema wakiwaita wengine Kituo cha Polisi
kwa vipimo, wamekuwa wakitumia dawa ya meno aina ya Colgate na chumvi,
lakini sasa wamekuja na mbinu mpya ya vipimo.
“Wengine tukiwaita kwa ajili ya vipimo,
kwa wale ambao wanapimwa kwa njia ya mdomo wanameza Colgate, wale
wanaopimwa kwa njia ya mkojo wanaweka chumvi.
“Mnakumbuka wengine tulipowaita walikuwa
wanachelewa kuja kumbe wanatumia vitu hivyo ili wasigundulike, sasa tuna
mbinu mpya za kuwapima,” alisema Makonda
No comments:
Write comments