Polisi waanza kumsaka aliyemtolea bastola Nape
Jeshi
la Polisi limesema limeanza kufanyia kazi maagizo waliyopatiwa na
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, kumsaka mtu
aliyemtolea bastola aliyekuwa Waziriri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo, Nape Nnauye.
Hayo yalisemwa jana na Msemaji wa Jeshi
hilo, Advera Senso. Awali, Mwananchi lilimtafuta Mkuu wa Jeshi hilo, IGP
Ernest Mangu, lakini simu yake ilipokelewa na msaidizi wake aliyemtaka
mwandishi amtafute Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Senso ili atoe
ufafanuzi kuhusu utekelezaji wa agizo la Waziri Nchemba.
Alipopigiwa simu, Senso alijibu kwa ufupi kuwa wameanza kufanyia kazi agizo la Waziri Nchemba.
“Sisi tumepokea maelezo ya waziri na tayari tumeanza kuyafanyia kazi, hilo ndilo ninaloweza kukwambia,” alisema.
Hali hiyo imekuja ikiwa ni siku moja
baada ya polisi aliyevalia kiraia kumtishia bastola, Nape ambaye pia ni
Mbunge wa Mtama (CCM).
Waziri Nchemba alilaani kitendo hicho na
kumuagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi kuchukua hatua “Mheshimiwa Nape sio
jambazi, hana rekodi za uhalifu. Kitendo cha kutolewa bastola si cha
Kitanzania na si cha kiaskari na sio cha Kimungu,” ameandika Mwigulu
katika ukurasa wake wa facebook.
“Kama mtu ameweza kutoa bastola mbele ya
kamera, nawaza mbali, ingekuwa kwenye uchochoro angefanya nini.
Nimemuagiza IGP achukue hatua.
“Nahusika na usalama wa raia wote wa
Tanzania. Nimemwelekeza IGP atumie picha kumsaka mtu yule aliyeinua
kufanya kitu cha kihalifu kwa kofia ya uaskari. Na kama ni askari, basi
sheria zinazoongoza taasisi husika zichukue mkondo wake.”
Credit – Mwananchi
No comments:
Write comments