Monday 27 March 2017

Watoto albino kurekebishwa viungo Marekani


Watoto wanne kutoka Tanzania wenye ulemavu wa ngozi (albino), wamepelekwa Marekani kurekebishwa viungo vya bandia walivyowekewa mwaka juzi nchini humo.

Kwa mara ya kwanza walipelekwa Marekani Julai mwaka juzi kwa ajili ya kuwekewa viungo bandia baada ya kushambuliwa kutokana na imani za kishirikina na kupoteza viungo vyao ikiwamo mikono, viganja na vidole.

Watoto waliokwenda Marekani mwaka huo walikuwa watano akiwamo msichana, Kabula Masanja kipindi hicho alikuwa na umri wa miaka 17, aliwekewa kiungo bandia baada ya mkono wake wa kulia kukatwa na watu wenye imani potofu.

Waliokwenda Marekani kwa mara ya pili ni Emmanuel Rutema (15), Baraka Lusambo (7), Mwigulu Magesa (14) na Pendo Noni (17 ambao waliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa John F. Kennedy, Machi 24 na walipokewa na mwanzilishi wa Taasisi ya Tiba (GMRF), Elissa Montanti.

Lusambo kwa mara ya kwanza alikwenda huko baada ya kukatwa kiganja cha mkono wa kulia, Rutema alikuwa amekatwa kiganja cha kushoto, baadhi ya vidole vya mkono wa kulia na kuharibiwa meno.

Mwigulu yeye alikuwa amekatwa mkono na aliwekewa wa bandia, hivyo watoto hao wanakwenda kurekebishiwa viungo hivyo, kwa kuwa umri na maumbile yao yamebadilika baada ya kukua.

GMRF ndiyo taasisi inayowatibu watoto wote waliojeruhiwa na kupoteza viungo vyao kutokana na vita au majanga.

Akizungumza mara baada ya kuwapokea watoto hao, Montanti alisema taasisi hiyo imepokea watoto zaidi ya 200 katika miaka 20 iliyopita, lakini wengi wanatokea Tanzania.

“Tumewasaidia watoto walioathirika na mambo mbalimbali ikiwamo mabomu, waliodhurika na majanga, lakini wanaotoka Tanzania ni wengi,” alisema Montanti

Watoto hao wanatarajiwa kukaa Marekani kwa miezi miwili, kupata tiba chini ya GMRF kwa kushirikiana na Hospitali ya Shriners ya Philadelphia.

Mfanyakazi wa shirika linalohudumia wenye ulemavu wa ngozi Tanzania la Under the Same Sun, Esther Rwela alisema watoto hao wanasoma kwenye shule ya bweni, (Safe House) na hawatoki nje mara kwa mara kwa sababu ya hofu.

“Wameathirika, bado wapo kwenye hofu na hawamuamini yeyote,” alisema Rwela.

Shirika la Umoja wa Mataifa linaeleza kuwa zaidi ya watu wenye ualbino 75 wameuawa katika nchi za Afrika Mashariki kati ya mwaka 2000 na 2015.

Kwa mujibu wa Ofisi ya UN inayosimamia Haki za Binadamu, viungo vya albino huuzwa kwa bei ya juu na hutumiwa kwa imani za kishirikina.

Ualbino umeathiri zaidi watu walio Kusini mwa Jangwa la Sahara, ambapo kwa upande wa Tanzania, katika kila watu 1,400 mmoja ana ulemavu huo.

No comments:
Write comments