Friday 17 March 2017

Watu wanataka chakula na siyo ndege – Rungwe


Mwenyekiti wa CHAUMMA, Hashim Rungwe Spunda ameishauri serikali kuweka mkazo zaidi katika kuhakikisha watanzania wanapa chakula, badala ya kuwekeza kwenye mambo mengine, ikiwemo ununuzi wa ndege.
Rungwe akiwa katika kipindi cha KIKAANGONI cha EATV, amesema kwa sasa nchini hali ni mbaya, na watanzania wengi wanasumbuliwa na njaa huku maisha yakizi kuwa magumu, na kuikumbusha serikali kuwa ilipaswa kutengeneza vituo vya afya vya kisasa vyenye madawa ya kutosha pamoja na kuhakikisha mahitaji muhimu ya wananchi yanapatikana na siyo kutumia fedha za umma kununulia ndege na ujenzi wa reli za treni za umeme ambazo haziwanufaishi watanzania wa kawaida.
“Mimi sikosoi mambo anayoyafanya Mh. Rais , Pesa za ndege ingekuwa ni mimi ningetengeneza vituo vya afya vya kisasa, madawa yangepatikana kwa wingi lakini pia majiko katika shule ili watoto wanywe uji, Unatengeneza reli  unabebaba nini ? umekuwa kuli wa nchi zingine, watu wako hawana chochote cha kusafirisha kwenda kuuza huko Afrika Mashariki” Alisema Rungwe
Amebainisha kuwa ndege zilizonunuliwa na serikali hivi sasa hazipati abiria kwa kuwa watu wana njaa, huku akitolea mfano siku moja aliposafiri katika ndege hiyo “Mimi mwenyewe wala sijasimulia, nilipanda ndege kutoka Dar kwenda Arusha, abiria walikuwa 18 tu, yaani ndege ya abiria 98 lakini inaondoka na abiria 18, mimi mwenyewe nimeshuhudia”
Aidha Rungwe amesema vijana wa taifa wanapaswa kushiriki katika suala la uzalishaji wa chakula na siyo kutelekezwa mitaani kitendo ambacho kinawapelekea ushawishi wa kujiingiza katika matumizi ya uvutaji wa bangi.
Hata hivyo Rungwe amesisitiza kwamba wananchi wana njaa hivyo serikali inawajibu wa kuhakikisha chakula kinakuwepo kingi kwa kuwa hilo ndilo jukumu lake hasa ikizingatiwa kwamba wananchi wanalipa kodi.
“Matatizo makubwa tuliyo nayo sisi nchini ni uongozi tu,  anayekusanya kodi ndiye mwenye kupanga pesa itumike vipi. Huwezi ukamwambia mtu akalime wakati hana vifaa atatumia mawe? Arudi kwenye stone age? Vijana wanaingia kwenye madawa kwa kukosa shughuli za kufanya”. Kauli ya Rungwe
Rungwe amesesema yeye angepatiwa nafasi ya kuongoza taifa la Tanzania kipaumbele cha kwanza kutoka kwake kingekuwa ni chakula ili wananchi waone tija ya kuishi kwenye nchi yao

No comments:
Write comments