Tuesday 4 April 2017

Idara uhamiaji yafumuliwa


KAMISHNA Jenerali wa Uhamiaji nchini, Dk Anna Makakala ameitikia agizo la Rais John Magufuli alilompa wakati akimwapisha Februari mwaka huu kuwa aifumue idara hiyo, jana alitangaza mabadiliko makubwa ya viongozi wa Uhamiaji wa mikoa mbalimbali nchini na kuwateua wakuu wapya wa mikoa Bara na Visiwani.

“Nakuagiza nenda ukafanye reform kubwa (mageuzi) kwenye eneo lako la kazi, pale kuna changamoto kuwa na tumegundua kuwepo na dosari nyingi,” alieleza Rais Magufuli alipomwapisha Dk Makakala, Februari 26, mwaka huu baada ya uteuzi wake akitokea kuwa Mkuu wa Chuo cha Uhamiaji Moshi mkoani Kilimanjaro.

Alitoa mfano kuwa mwaka jana, Tanzania ilipata ugeni wa waumini wa madhehebu ya Mabohora waliofanyia sherehe yao kubwa nchini. Alisema sherehe hizo kwa kuwa zilikuwa za kimataifa wageni wapatao 32,000 waliingia nchini kuja kusherehekea sikukuu hiyo.

Alisema ukipiga hesabu ya kila mmoja ni wazi kuwa walilipa fedha za kutosha; lakini cha ajabu ni kwamba alipouliza fedha kiasi gani zilipatikana kutokana na ugeni huo mkubwa, hadi leo hajapatiwa hesabu yoyote jambo linalodhihirisha kwamba kuna matatizo makubwa katika Idara ya Uhamiaji.

“Kwa hiyo Kitengo cha Fedha pale Uhamiaji kuna matatizo makubwa, nenda ukafanye mabadiliko. Nimechagua mwanamke kwa kuwa naamini kwamba wanawake ni waaminifu, kwa hiyo kufeli kwako ni kufeli kwa wanawake wote, nenda ukafanye mabadiliko, usiogope sura, tutataka ukafanye total reform (mageuzi makubwa), not partial reform (mageuzi nusu),” alisema Rais Magufuli.

Kabla ya mabadiliko makubwa ya jana, Dk Makakala aliteua makamishna sita ambao ni Peter Chogero ambaye ni Kamishna wa Divisheni ya Fedha na Utawala, Samwel Magweiga (Kamishna wa Divisheni ya Udhibiti na Uongozi na Mipaka), Gerald Kihiga (Kamishna wa Divisheni ya Pasipoti na Uraia), Musanga Etimba (Kamishna wa Divisheni ya Hati za Ukaazi na Pasi) na Hannerole Manyanga ambaye ni Kamishna wa Divisheni ya Sheria.

Lakini jana, Dk Makakala alitangaza mabadiliko mengine makubwa ambayo yameshuhudia Naibu Kamishna wa Uhamiaji, Sixtus Nyaki aliyekuwa Mkuu wa Uhamiaji Mkoa wa Mwanza akihamishiwa Mkoa wa Simiyu wakati aliyekuwa Mkuu wa Uhamiaji Mkoa wa Rukwa, Naibu Kamishna wa Uhamiaji Selemani Kameya amehamishiwa Tabora.

Taarifa iliyotolewa na Kamishna Jenerali huyo inaonesha kuwa Mkuu wa Uhamiaji Mkoa wa Mbeya, Naibu Kamishna wa Uhamiaji Asumsio Achacha amehamishiwa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Mkuu wa Uhamiaji Mkoa wa Manyara, Naibu Kamishna Peter Kundy amehamishiwa Mkoa wa Dodoma kuchukua nafasi ya Kamishna Msaidizi, Ali Mohamed ambaye amehamishiwa kuwa Mkuu wa Uhamiaji Mkoa wa Arusha.

Aidha, Naibu Kamishna wa Uhamiaji Mkemi Seif ameteuliwa kuwa Mkuu wa Uhamiaji Mkoa wa Kusini Unguja, Naibu Kamishna wa Uhamiaji, Muhsin Abdallah Muhsin ameteuliwa kuwa Mkuu wa Uhamiaji Mkoa wa Kaskazini Unguja, Naibu Kamishna wa Uhamiaji, Said Omary Hamdani ameteuliwa kuwa Mkuu wa Uhamiaji Mkoa wa Mjini Magharibi na Naibu Kamishna wa Uhamiaji Othman Khamis Salum ameteuliwa kuwa Mkuu wa Uhamiaji Mjini Magharibi Unguja.

Pia baadhi ya wakuu wa Uhamiaji wa mikoa wamebaki katika vituo vyao vya kazi vya awali akiwemo Mkuu wa Uhamiaji Mkoa wa Morogoro, Naibu Kamishna wa Uhamiaji Safina Muhindi, Mkuu wa Uhamiaji Mkoa wa Lindi, Naibu Kamishna wa Uhamiaji George Kombe, Mkuu wa Uhamiaji Mkoa wa Ruvuma, Naibu Kamishna wa Uhamiaji Hilgaty Shauri, Mkuu wa Uhamiaji Mkoa wa Singida, Naibu Kamishna wa Uhamiaji Faith Ihano na Mkuu wa Uhamiaji Mkoa wa Mara, Naibu Kamishna Fredrick Kiondo.

Wamo Naibu Kamishna wa Uhamiaji, Abdallah Towo (Kagera) na Naibu Kamishna wa Uhamiaji Anastazia Ngatunga (Shinyanga). Taarifa hiyo iliongeza kuwa Dk Makakala pia amewateua viongozi wa Uhamiaji wa mikoa wapya katika baadhi ya mikoa nchini ambapo Naibu Kamishna wa Uhamiaji, Mary Palmer ameteuliwa kuwa Mkuu wa Uhamiaji Mkoa wa Dar es Salaam, Naibu Kamishna wa Uhamiaji, Plasid Mazengo (Pwani), Mrakibu Mwandamizi wa Uhamiaji James Mwanjotile (Mtwara), Kamishna Msaidizi Mwandamizi Hope Kawawa (Iringa), na Kamishna Msaidizi wa Uhamiaji Hosea Kagimbo (Njombe).

Wengine ni Naibu Kamishna wa Uhamiaji Rashid Magetta (Songwe), Naibu Kamishna wa Uhamiaji Carlos Haule (Rukwa), Naibu Kamishna wa Uhamiaji Julieth Sagamiko (Manyara), Naibu Kamishna wa Uhamiaji Albert Rwelamila (Kilimanjaro) na Naibu Kamishna wa Uhamiaji Paul Eranga (Mwanza).

Naibu Kamishna wa Uhamiaji Crispin Ngonyani (Tanga), Naibu Kamishna wa Uhamiaji Shaaban Hatibu (Katavi), Naibu Kamishna wa Uhamiaji Remigius Pesambili (Kigoma) na Mrakibu Mwandamizi wa Uhamiaji Novaita Mrosso (Mbeya).

Aidha, Mrakibu Mwandamizi wa Uhamiaji Bakari Mohamed Ameir ameteuliwa kuwa Mkuu wa Kituo cha Uhamiaji cha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, Zanzibar na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhamiaji Fulgence Mutarasha kuwa Mkuu wa Uhamiaji Kituo cha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam.

Bosi mpya aifumua idara ya Uhamiaji Inatoka Uk. 1 Wapinzani wavurunda Na Magnus Mahenge, Dodoma OFISI ya Bunge imeshindwa kuteua wagombea wa vyama vya upinzani kwa ajili ya uchaguzi wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) unaofanyika leo baada ya kukiuka kanuni za uchaguzi huo na vimepewa hadi leo saa saba mchana kurekebisha upungufu kwenye fomu mbalimbali za wagombea.

“Kutokana na upungufu huo, msimamizi wa uchaguzi nimeshindwa kuteua wagombea wa kundi hilo, hivyo nimeviandikia vyama vyenye haki ya kugombea kuvitaka kurekebisha upungufu ulioainishwa na kuwasilisha majina na nyaraka zinazohitajika ofisini kwangu Dodoma Aprili 4, mwaka huu kabla ya saa saba mchana,” alisema Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah.

Dk Kashililah ambaye ni Msimamizi wa Uchaguzi huo, alisema Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Chama cha Wananchi (CUF) havikuzingatia masharti ya Ibara ya 50 ya Mkataba wa Kuanzishwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), inayotaka theluthi moja ya wabunge tisa izingatie jinsia zote mbili.

CCM ndicho chama pekee ambacho kimewasilisha orodha ya nyaraka zinazoonesha wagombea wake wote wamekidhi vigezo na masharti ya uchaguzi wa kuwa wabunge wa EALA. Alisema Chadema haijazingatia jinsia ili kuwezesha utekelezaji wa masharti ya kifungu namba 4 (4) cha sheria ya wajumbe wa EALA ya angalau theluthi moja ya wajumbe zioneshe jinsia zote mbili.

Pia alisema haijawasilisha fomu za wagombea, orodha ya waombaji haipo na fomu za matokeo ya kura zilizopigwa hazipo. Hata hiyo, Ofisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene alidai hakuna utaratibu wowote uliokiukwa kwa wao kuteua wagombea wa nafasi za ubunge wa Bunge la Afrika Mashariki isipokuwa msimamizi wa uchaguzi, Dk Kashililah ameamua kuja na utaratibu wake anaoujua mwenyewe, hivyo walitarajia kutoa msimamo wao jana jioni.

“Hakuna taratibu zilizokiukwa katika kuteua wagombea wetu wa kugombea ubunge wa EALA, isipokuwa msimamizi wa uchaguzi, Dk Kashililah ameamua kutoa msimamo wake mwenyewe, sisi tutatoa msimamo wetu jioni ya leo (jana),” alidai Makene. Naye Kaimu Katibu Mkuu wa CUF, Magdalena Sakaya amesema chama hicho kina imani na Spika Job Ndugai kuwa atafuata sheria na kanuni za uchaguzi kwa kutambua CUF ni moja na haina vipande vipande hasa katika suala la wagombea wa Afrika Mashariki.

Alisema wanaamini Spika atatenda haki katika suala la wagombea ubunge wa Bunge la Afrika Mashariki kwa kuamini CUF ni moja na haiko vipande vipande. Uteuzi ndani ya CUF haujazingatia jinsia ili kutekeleza masharti ya kifungu namba 4 (4) sheria ya uchaguzi wa wajumbe wa Bunge hilo ambayo inataka kati ya wabunge tisa ioneshe uwepo wa jinsia zote.

Alisema fomu za uteuzi wa wagombea zimewasilishwa na mamlaka mbili tofauti, wagombea wawili hawana uthibitisho wa uraia, orodha ya waombaji haipo kwa mgombea mmoja, fomu ya matokeo ya kura kwa wagombea wote haipo na fomu ya mahudhurio kwa mgombea mmoja haipo.

“Uteuzi wa wagombea wa kundi C wa vyama vya upinzani utafanyika Aprili 4, mwaka huu, wakati wowote kuanzia saa saba kamili mchana mara baada ya kupokea na kuchambua nyaraka zitakazowasilishwa kwangu na vyama husika,” alieleza Dk Kashililah.

Kutokana na mamlaka aliyopewa, Msimamizi wa Uchaguzi alitangaza na kutoa taarifa kwa umma kwamba waliokidhi vigezo na masharti ya kuteuliwa kugombea kwenye uchaguzi wa wajumbe wa EALA uliopangwa kufanyika leo.

Wagombea waliokidhi vigezo kutoka kundi A la wanawake ni Happiness Lugiko (CCM) na Zainabu Kawawa (CCM), kundi B la wanaume Tanzania Bara ni Adam Kimbisa, Anamringi Macha, Charles Makongoro, Dk Ngwalu Maghembe, Fancy Nkuhi na Happiness Mgalula na wagombea wa kutoka Zanzibar ni Abdullah Husna Makame, Maryam Ussi Yahya, Mohamed Yusufu Nuhu na Rabia Abdallah Hamid.

Wagombea wa vyama vya upinzani ambao hawajakidhi vigezo ni Ezekiel Wenje na Lawrance Masha (Chadema), Habibu Mohammed Mnyaa, Sonia Jumaa Magogo, Thomas Malima na Twaha Taslima (CUF).

Wengine ni Nderakindo Perpetua Kessy (NCCR-Mageuzi) na Profesa Kitila Mkumbo (ACT-Wazalendo), Majina ya wagombea hao yaliwasilishwa na vyama vyao tangu Machi 30, mwaka huu kabla ya saa 10 jioni kama masharti ya kanuni ya 5 (4) ya nyongeza ya tatu ya kanuni za kudumu za Bunge toleo la Januari 2016.

Baada ya hatua hiyo, uchambuzi ulifanyika kwa kuzingatia ibara ya 50 ya mkataba, ibara ya 67 ya Katiba ya Jamhuri ya mwaka 1977, sheria ya uchaguzi wa wa wajumbe wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) na kubaini upungufu kwa vyama hivyo.

Dk Kashililah aliwapongeza wagombea waliojitokeza katika nafasi mbalimbali wanaofikia 505, CCM (471), Chadema (17), CUF (8), NCCR-Mageuzi (3) na ACT-Wazalendo (6). Wagombea hao walichujwa na vyama vyao na kubakiza majina 20 kugombea ambao ni CCM (12), Chadema (2), CUF (4), NCCRMageuzi (1) na ACT-Wazalendo (1).

Katika wagombea hao, wanaume ni 12 na wanawake ni wanane, CCM (wanawake 6 na wanaume 6), Chadema mwanamke mmoja na wanaume wawili, CUF mwanamke mmoja na wanaume watatu, NCCR-Mageuzi mwanamke mmoja na hakuna mwanamume na ACT-Wazalendo hakuna mwanamke na mwanamume ni mmoja.

Uchaguzi huo ukikamilika watapatikana wabunge tisa wa kuwakilisha Tanzania kwenye Bunge la Afrika Mashariki lenye makao yake makuu Arusha. Katika orodha hiyo, wabunge wa CCM watakuwa sita na wabunge wa upinzani watatu.

Shughuli zikiendelea kama kawaida katika Kituo Kikuu cha Mabasi ya Mikoani Ubungo, Dar es Salaam jana baada ya mgomo uliokuwa ufanywe na wasafirishaji wa abiria kupatiwa ufumbuzi baada ya mazungumzo baina ya serikali na wamiliki wa mabasi nchini. 

No comments:
Write comments