Sunday, 2 April 2017

Zuio la pikipiki usiku ni la muda mfupi - Ndikilo


Rufiji. Siku nne tangu kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa wa Pwani kutoa agizo la kusitisha usafiri wa pikipiki kuanzia saa 12:00 jioni ili kudhibiti matukio ya mauaji, Serikali imesema zuio hilo ni la muda mfupi na wananchi wanapaswa kulitii.

Akizungumza na gazeti hili jana kuhusu agizo hilo lililoibua malalamiko kutoka kwa wafanyabiashara na wananchi wakidai polisi wanawalazimisha kufunga maduka, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo alisema amri hiyo inatokana na taarifa za kiintelijensia kuhusu matukio ya mauaji.

Ndikilo alisema kipindi hiki ni kigumu, hivyo wananchi wanapaswa kutii sheria kama wanavyoamriwa na vyombo vya dola kwa kuwa baada ya muda mfupi hali itarejea kama ilivyokuwa awali.

Akizungumzia ufanisi wa operesheni ya kuwakamata watu wanaojihusisha na mauaji ya viongozi katika wilaya za Kibiti, Rufiji na Mkuranga, alisema ina maendeleo mazuri kwa kuwa watu kadhaa wanashikiliwa na polisi kwa mauaji ya viongozi wa Serikali za Mitaa.

Ndikilo alitoa wito kwa wananchi wa wilaya za Kibiti, Rufiji na Mkuranga kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi ili kufanikisha kazi ya kuwakamata watu wote wanaojihusisha na mauaji.

Tangu Machi 29 lilipotolewa agizo la kuzuia bodaboda kufanya kazi baada ya saa 12:00 jioni wilayani Rufiji, kumeibua malalamiko kutoka kwa wafanyabiashara na wananchi wakilituhumu Jeshi la Polisi kuwalazimisha kufunga maduka, kuzuia usafiri wa baiskeli na kuwataka wasitembee zaidi ya saa mbili usiku.

Mfanyabiashara wa Ikwiriri, Moshi Tindwa alisema kutokana na amri ya kuwataka kufunga mapema maeneo yao ya biashara, mauzo yameshuka.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Onesmo Lyanga alisema hana taarifa kuhusu malalamiko hayo.

“Sina taarifa zozote juu ya malalamiko hayo, kama kuna mwenye malalamiko anieleze.” alisema.

No comments:
Write comments