Saturday 27 May 2017

KIVULI CHA MANJI CHAENDELEA KUITESA YANGA


Kuondoka kwa Mwenyekiti wa Yanga, Yusuph Manji kumeonekana kuanza kuitesa klabu hiyo kuanzia kwa viongozi, wanachama na wachezaji wa timu hiyo.
Manji ambaye aliandika barua ya kujiuzulu nafasi yake hiyo ndani ya klabu hiyo, ameacha simanzi kubwa, huku athari zake zikianza kuonekana kwenye usajili.
Tayari Yanga imemkosa kiungo iliyokuwa ikimhitaji tangu msimu uliopita , Kenny Ally aliyekuwa akiichezea Mbeya City.Ilionekana kama tayari Yanga ilimaliza mchezaji, lakini haikuwa hivyo.
Akiwa mfadhili na mwenyekiti, ilikuwa si rahisi kwa Yanga kumkosa mchezaji yoyote inayomhitaji ndani na nje ya nchi.
Kenny kwa sasa ametua kwenye klabu ya Singida United kwa mkataba wa miaka miwili na kuipiga bao timu hio.
“Yanga waliongea na mimi, lakini naona hawakuwa ‘siriasi’, lakini Singida wao walikuja moja kwa moja wakamaliza kazi, ndiyo maana unaona nimesajili miaka miwili,” alisema mchezaji  huyo.
Inawezekana ikawa ni mwanzo tu, kwani huenda Yanga ikapata shida kipindi hiki cha usajili kutokana na mazoea ya wachezaji wengi wa sasa kutaka pesa nyingi, hasa wanapotakiwa na timu hiyo na Manji alikuwa akitoa bila wasiwasi.
Lakini pia viongozi wa matawi wa klabu hiyo walikutana haraka na kuazimia kumtaka kiongozi wao huyo asijiuzulu, badala yake apumzike tu halafu baadaye arejee kwenye kiti chake.
Manji alijiuzulu kwa kile alichosema kuwa ameshauriwa na daktari wake.

No comments:
Write comments