WAWKILI Tundu
Lissu na wenzake wa Chama Cha Wanasheria Tanganyika (TLS) wamelikomalia
vilivyo sakata maarufu la Bashite linalohusiana na tuhuma za kughushi
vyeti vya kielimu linalomkabili mmoja wa wakuu wa mikoa kwa kulifikisha
kortini ili lipatiwe ufumbuzi.
Aidha,
Lissu na wenzake hao wamedhamiria kuona kuwa kigogo huyo anayetuhumiwa
kuliacha jina lake halisi la Daudi Albert Bashite kutokana na matokeo
mabovu ya sekondari na kutumia jina la mtu mwingine, achukuliwe hatua za
kisheria ikiwamo kufungwa jela kwa kosa la kughushi ikiwa itathibitika
kuwa ana hatia.
Akizungumza
jana na waandishi wa habari mjini Dodoma jana, Lissu ambaye ni Rais wa
TLS, alisema uamuzi huo wa kulifikisha mahakamani suala la Bashite
umetokana na maazimio ya baraza la uongozi la chama hicho, lengo likiwa
ni kulinda utawala wa sheria na uwajibikaji nchini.
Tofauti
na matarajio ya baadhi ya watu, sakata hilo la Bashite halikupatiwa
jibu kutokana na ripoti ya uhakiki wa vyeti vya watumishi wote wa umma
iliyokabidhiwa kwa Rais John Magufuli Ijumaa kutowagusa viongozi wa
kisiasa wakiwamo mawaziri, wakuu wa mikoa, wabunge na madiwani.
Katika
kufanikisha nia hiyo ya TLS, Lissu aliyekuwa na viongozi wengine wa
chama hicho wakiwamo Makamu Rais, Godwin Ngwilimi na Wakili Stephen
Kuwayawaya, alisema miongoni mwa hatua walizochukua ni pamoja na TLS
kufungua mashtaka binafsi ya jinai dhidi ya mkuu huyo anayedaiwa kuitwa
Bashite.
Aliongeza
kuwa mkuu huyo wa mkoa, anatuhumiwa kwa makosa mbalimbali ya jinai
likiwamo hilo la kutumia vyeti feki na kwamba, kazi ya kumshtaki
haitachukua miezi bali ni wiki mbili au tatu.
“Kifungu
cha 128(2) cha sheria ya Mwenendo wa jinai, sura ya 20 ya sheria za
Tanzania kinaruhusu mtu binafsi (pamoja na taasisi, kampuni au mashirika
kama TLS) kupeleka malalamiko kwa hakimu mwenye mamlaka pale anapoamini
kuna sababu za msingi zinazoonyesha kuwa kosa la jinai
limetendwa,”alisema Lissu, akielezea vifungu wanavyotumia kufikisha
suala hilo kortini.
Alisema
dhana ya utawala wa sheria ina maana pana na kwamba, pamoja na mambo
mengine, siyo tu kwamba hakuna mtu aliyeko juu ya sheria, bali pia kila
mtu bila kujali cheo au nasaba na hali yake kiuchumi na jamii, yuko
chini ya udhibiti wa sheria za kawaida za nchi na hivyo yuko pia chini
ya mamlaka ya mahakama za kawaida.
“Kuna
tuhuma za muda mrefu sasa kwamba Mkuu huyo wa mkoa ametumia vyeti vya
shule ya sekondari visivyokuwa vyake. Yeye… ni Daudi (Albert) Bashite,”
alisema Lissu, akiongeza kuwa jina linalotumiwa sasa na mkuu huyo
linadaiwa kuwa mwenyewe yupo na ndiye mwenye vyeti halisi, na kitendo
hicho ni kosa la jinai.
Akifafanua
zaidi, Lissu alisema kifungu cha 120 cha Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16
ya Sheria za Tanzania, kinasema “Mtu yeyote aliye kwenye utumishi wa
umma ambaye, wakati akitekeleza majukumu ya ofisi yake akifanya kitendo
cha udanganyifu au ukiukaji dhamana huo ungekuwa ni kosa la jinai kama
ungefanywa na mtu binafsi au la, anafanya kosa na endapo atapatikana na
hatia atapata adhabu ya kifungo cha miaka saba jela.”
Lissu
alisema kwa kutumia vyeti vya shule visivyokuwa vyake, na kwa kutumia
majina ya mtu mwingine wakati akiwa mtumishi wa umma, mkuu huyo mwenye
jina halisi la Daudi Bashite ameathiri imani ya wananchi kwa serikali
yao kwa kuajiri na kulinda watu wadanganyifu na wasiokuwa na vyeti
halali.
“Mtu
huyu amefanya kosa la jinai ambalo kwalo anastahili kushtakiwa
mahakamani na endapo atapatikana na hatia anastahili kuadhibiwa kwa
mujibu wa sheria za kawaida za nchi yetu,” alisema Lissu ambaye pia ni
Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema).
Lissu
aliongeza kuwa endapo Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) atakataa kutoa
ridhaa, TLS itamfungulia mkuu huyo wa mkoa mashataka ya rejea ya
kimahakama katika Mahakama Kuu ili alazimishwe kutoa ridhaa hiyo.
Kabla
ya kumkabidhi Rais Magufuli ripoti ya uhakiki wa vyeti vya elimu na
kitaluma kwa watumishi wa umma nchini, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais
Utumishi na Uatawala Bora, Angela Kairuki, alisema watumishi 9,932
walikutwa na vyeti vya kughushi na kwamba, ripoti hiyo haikuwagusa
viongozi wa kisiasa wakiwamo mawaziri, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya,
wabunge na madiuwani.
Hata
hivyo, Makamu Rais wa TLS, Ngwilimi, alisema kuwa kwa mujibu wa kifungu
cha Sheria ya Utumishi wa Umma namba 3 na 5, tafsiri ya mtumishi wa
umma inawahusisha pia Wakuu wa mikoa na Wakuu wa Wilaya na hivyo kina
Bashite walipaswa pia kuhusishwa katika uhakiki huo.
No comments:
Write comments