Saturday 3 June 2017

IMEVUJA;SIMBA KUWASAJILI HAWA


Kwanza kabisa nitoe pongezi za dhati kwa uongozi, wanachama , wapenzi na mashabiki wandamizi wa klabu hii ya pili kwa ukongwe nchini ikianzishwa mwaka 1936 mwaka mmoja baada ya mahasimu wao wakubwa Yanga SC kuanzishwa mwaka 1935. Pongezi zangu zinalenga katika ushindi wao wa kombe la FA nchini ( ASFC ) ambao limewapatia tiketi ya kushiriki michuano ya kombe la Shirikisho mwakani.
Ni dhahiri shayiri wanastahili pongezi baada ya kukaa nje ya uringo wa soka la kimataifa kwa takribani miaka mitano ingawa licha ya muda wote huo, bado legacy yao kimataifa ni kubwa katika nchi hii.
Simba SC wanashikiria rekodi maridhawa ya kucheza fainali za michuano ya CAF mwaka 1993 michuano ambayo ilibadirishwa na kuitwa washindi barani Afrika . Sambamba na hilo wana kumbukumbu nzuri ya kumng’oa bingwa wa Afrika Zamaleki mwaka 2003 katika michuano ya klabu bingwa Afrika kitu ambacho hakijawahi kufanywa na klabu yoyote nchini.
Ni washindi mara sita! wa kombe la Kagame ( CECAFA ) rekodi ambayo bado haijavunjwa na klabu yoyote ile ukanda wa Afrika mashariki na kati ingawa Gor Mahia na Yanga SC wanainyatia rekodi hiyo kwa kuchukua kombe hilo mara tano kila mmoja.
Dibaji hiyo juu itazidi kutuonesha ugwiji wa klabu hii katika soka la kimataifa licha ya kukaa nje kwa muda mrefu . Kurudi upya katika uringo huu ni ujio mpya wa kuvunja na kuweka rekodi zake mpya ? muda utatoa hukumu katika hilo.
Kwa zaidi ya misimu mitatu hususani msimu wa 2012-13 na 2013-14 Simba SC walikuwa katika ujenzi wa timu baada ya kuondokewa na nyota wake wengi ambao waliipa mafaniko klabu hiyo kwa misimu kadhaa hususani 2007 mpaka 2011 ambapo Simba SC walifanikiwa kulitwaa kombe la ligi kuu mara tatu (3) yaani 2007, 2009-10 na 2011-12.
Baada ya mafanikio hayo Simba SC ilipoteza wachezaji wake wengi mahiri hali iliyowafanya kwa zaidi ya miaka mitano kukaa kimya kimataifa wakijenga timu yao . Mwaka 2012 tu, walipata pigo kwa kumpoteza kiungo wao mahiri Patrick Mafisango kwa ajali ya gari mchezaji ambaye anakumbukwa sana kati ile mechi ya Simba SC ana shinda 5-0 dhidi ya Yanga mwaka 2012 akishikiria vilivyo eneo la kiungo.
Kumbuka kikosi cha Simba 2011 kilichotoweka ambacho kimsingi kinasinama kama alama ya mafanikio ya klabu hiyo ya mwisho kabla ya juzi kufuzu kombe la Shirikisho kwa kuifunga Mbao FC 2-1 mchezo wa fainali ASFC. Kikosi kilichokuwa kikiwajumuisha golikipa Juma Kaseja akizungukwa na walinzi kama Juma Jabu , Nyoso , Kanoni na Kelvin Yondani.
Safu ya kiungo unawakuta Jerry Santosi , Mafisango na Patrick Ochan .
Washambuliaji Emanuel Okwi, Mbwana Samata na Musa Mgosi akiwa katika kiwango kizuri kabisa cha kucheka na nyavu .
Wengine ni Shija Mkina , Meshack Abel , Ali Ahmed Shiboli na wengineo . Ni kikosi cha mwisho katika mafanikio ya Simba SC hususani kuanzia 2011-12 . Wachezaji ambao waliitoa kamasi TP Mazembe uwanja wa taifa licha ya ushindi wa 3-2 .
Baada ya hapo utaona wachezaji hawa wengi waliondoka hapo klabuni na Simba kuanza kujengww upya hususani msimu wa Kibadeni na Julio wakitumia wachezaji wengi wapya wa Simba B mfano kina Ndemla , Singano , Seseme na wengineo.
Tactical build up na ujio wa Azam FC kwa kiasi fulani uliwafanya Simba SC kupotea katika anga za kimataifa na kila uchao kuanza upya kwenye kada ya wachezaji na makocha .
Chanzo cha mafaniko 2016-17…..
Kama unakumbuka moja ya kituko kikubwa msimu uliopita wa 2015-16 ni pale mwenyekiti wa kamati ya usajili ya Simba SC na mjumbe wa kamati kuu ndugu Hans Poppe alipokuwa akizuiwa na mashabiki wa Simba SC asitoke uwanja wa taifa baada ya timu yao kupoteza mchezo wa robo fainali dhidi ya Coastal Union . Mashabiki wakimrushia maneno makali yeye na viongozi wenzake waiache timu yao kwa kushindwa kuipa mafanikio . Alizunguka na gari kwa fujo ili wampishe njia .
Kitendo hicho na ishara nyingi za mashabiki wa klabu hiyo iliyopata kuvuma sara katika anga la soka la nchi hii na kimataifa mpaka kufikia kuitwa ‘ TAIFA KUBWA ‘ ndio viliwafanya viongozi wa Simba SC kukaa chini na kutafakari kwa kina nini cha kufanya kuirudishia heshima klabu hiyo .
Mabadiliko benchi la ufundi..
Msimu wa 2015-16 ni kama Simba SC walikuwa na mzaha tu. Jackson Mayanja alisimama peke yake kwenye benchi la ufundi na kukosa wasaidizi makini kumshauri na kumsaidia kuiweka vyema timu hiyo kimbinu. Lakini mabadiliko waliyofanya msimu huu wa 2016-17 yameonesha ni watu makini na nini wanakitaka katika soka la nchi hii.
Kumleta Joseph Omog kama kocha mkuu na kumshawishi Mayanja kubaki ni moja ya maamuzi mazuri waliyoyafanya na mafanikio wameyaona kwa kubeba kombe la ASFC na kulingana alama na bingwa wa ligi kuu Yanga SC kwa tofauti ya magoli ya kufungwa na kufunga . Hii ni tofauti na misimu mitatu nyuma ambapo walikuwa wakimaliza ligi nafasi ya tatu au ya pili wakiwaacha Yanga na Azam wakitaradadi kimataifa.
Joseph Omog ni mwalimu mzoefu katika soka la Afrika. Raia huyu kutoka nchini Cameroon aliipa ubingwa Azam FC msimu wa 2013-14 katikati ya miamba ya soka Tanzania Yanga SC na wao Simba SC . Moja ya falsafa yake ni ubora wa timu katika eneo la ulinzi na kiungo huku akishambulia aidha kwa viungo wanaosimama kama ‘ washambuliaji vificho ‘ au viungo kutengeneza mfumo mzuri wa washambuliaji wao kushambulia.
Sambamba na uwezo kimbinu pia ni mzuri kusimamia nidhamu ya mchezaji uwanjani na nje ya uwanja pia kusoma tempo ya mchezo na kuubadili katika mafaniko yake . Tazama mechi zote mbili dhidi ya watani zao wa jadi Yanga SC alivyozicheza kimbinu na kiufundi.
Kumwacha Mayanja kwenye timu ulikuwa mwendelezo mzuri wa mbinu zake na falsafa zake katika timu hiyo ambazo alianza kuzijenga toka akiwa kocha mkuu msimu wa 2015-16 hivyo kombinesheni yake na Omog imetoa matokeo chanya . Mayanja akisimama kama mwenyeji ndani ya timu na Omog akitumia fursa hiyo kuijua timu na jinsi gani ya kupenyeza mbinu na falsafa zake.
Mabadiliko ya kikosi….
Msimu wa 2015-16 Simba SC ilitawaliwa na wachezaji wengi ambao walikuwa wanashindwa kudumu na vipaji vyao kwa muda mrefu , nidhamu bora ndani ya uwanja na nje ya uwanja. Kamati ya Ufundi ya ikiongozwa na kocha mkuu wa Simba SC wakati huo Jackson Mayanja ilifanya usajili mzuri sana msimu huu . Naweza sema ni usajili ambao umechangia kuirudishia Simba SC meno na makucha yake ambayo yalimwezesha kuitwa ‘ Taifa Kubwa ‘.
Usajili ulilenga kuleta wachezaji wenye vipaji vizuri, nidhamu, uzalendo na kazi yake pia klabu na wenye kiu ya mafaniko.
Shiza Kichuya na Mzamiru Yassin toka Mtibwa Sugar wanakufungua vyema katika hili ninaloliangazia. Ubora wao kila mmoja kauna na kuukubali kwa asilimia nyingi tu . Ni vijana wadogo wenye kiu ya mafanikio na muda wote wakivaa jezi ya Simba SC unaiona mishipa ya uzalendo ikisimama vichwani mwao .
Mfumo mzima wa timu kiulinzi na kiushambuluaji ( offensive and defensive patterns ) za mwalimu Joseph Omog kwa msimu wa 2016-17 aliusuka kuwazunguka hawa watu.
Kukosa mbadala wa namba tatu nje ya Mohamedi Hussein ‘ Zimbwe Jr ‘ na kuamua kulinda kipaji chake na nidhamu yake kitu ambacho kilimwezesha mchezaji huyo kucheza mechi zote 30 katika kiwango kizuri na kuambulia kadi moja tu ya njano , ni kongole nyingine kwa waalimu na alama ya mafanikio ya klabu hiyo kwa msimu huu .
Achana na tuzo ya uchezaji bora aliyopata mchezaji huyu , Zimbwe anawakilisha uwezo wake binafsi na waalimu wake katiba ubanifu wa nguvu na uwezo wa kutumia rasilimali zilizopo kuleta mafaniko.
Besala Bukungu na Methodi Mwanjali ni uchaguzi bora wa wachezaji wakongwe wenye nidhamu, haiba ya uongozi kwa wenzao , uzoefu na kipaji halisi kuipa timu mafanikio. Usajili wao ni tija na ufanisi mkubwa msimu huu.
Jicho la tatu katika usajili wa dirisha dogo hususani kuchukua maamuzi magumu ya kumuondoa kikosini golikipa namba moja wa klabu hiyo Angban na kumtoa kwa mkopo Blagnon kuliifanya Simba kukaa kimbinu na kiufundi. Ujio wa Daniel Agyei kama mbadala wa Angban ulikuwa sahihi . Ni golikipa kijana na mwenye uwezo mkubwa na amelilinda vyema lango la Simba SC mzunguko wa pili wa ligi kuu.
James Kotei eneo la kiungo ameleta changamoto kubwa kwa Jonasi Mkude ambaye alianza kusuguana na uongozi kutokana na sababu mbalimbali na kuhatalisha ufanisi wa klabu kiufundi katika eneo hilo . Hali ya uthubutu kuleta kiungo mwingine licha ya ubora wa Mkude , lilikuwa somo kubwa kwa Mkude na wachezaji wengine kuelewa dhumuni la klabu msimu huu na umakini walionao . Mwisho wa siku Kotei akatengeneza kombinesheni nzuri na Mkude pia kuna wakati akisimama kama mlinzi wa kati .
Ingawa hawajafanikiwa sana kwa mshambuliaji Laudit Mavugo hususani katika rekodi yake ya ufungaji wakimsajili kwa tumaini kubwa toka Vitalo O ya Burundi ambapo alikuwa na rekodi ya kufikisha magoli 30 kwa msimu, bado mchezaji huyo amewafungia magoli muhimu katika michuano ya ASFC.
Ndio mchezaji aliyewavusha hatua zote za robo fainali na nusu fainali kwenda fainali akifunga goli pekee dhidi ya Madini FC jijini Arusha. Mavugo magoli 6 tu katika msimamo wa ligi kuu lakini ni mmoja wa wachezaji ambao waliifanya Simba kuogopwa msimu huu kutokana na rekodi yake ya kucheka na nyavu.
Ukaribu wa wanachama na viongozi wa klabu hiyo pia umechangia kwa asilimia kubwa kuipa mafanikio klabu hiyo msimu huu . Wanachama walikuwa wakichanga fedha za motisha kila mechi ili kuwapa nguvu wachezaji wao . Yote hii inaonesha umakini ambao Simba SC waliuweka msimu huu.
Lakini katika hili huwezi kumsahau bilionea Mohamedi Dewji aliyeamua kuibeba klabu hiyo mabegani mwaka ili kushinda na kupata fursa ya kuiwakilisha nchi Kimataifa. Aliamua kuchukua jukumu la kulipa mishahara ya makocha na wachezaji kitu ambacho kiliongeza ari na moyo wa kupambana kwakuwa na uhakika wa malipo wa kazi yao.
Mustakabali wa Simba SC 2017-18
Ni wakati sasa kama klabu kukaa chini na kujitafakari kwa neema hii waliyoipata ya kuiwakilisha nchi kimataifa mwakani katika kombe la Shirikisho. Tafakari kuhusu usajili makini , mfumo bora wa uendeshaji klabu na mipango sahihi ya kuimarisha misuli ya kiuchumi ya klabu ili uwakilishi wao uwe wenye tija na kuziendeleza rekodi zao bora kimataifa.
Usajili…
Naanza kwa kuiangazia nafasi ya walinda milango wa Simba SC . Bado wanahitaji huduma ya Daniel Agyei. Ni golikipa mwenye uwezi mkubwa na atawafaa kitaifa na kimataifa lakini ni wakati sasa wa kumfungulia mlango wa kutokea Manyika Jr. Kijana mdogo mwenye kipaji lakini ameshindwa kutunza kipaji chake kwakuwa na mambo mengi nje ya uwanja . Mbadala wa Manyika kwa hapa nchini ni Aishi Manula wa Azam FC au Youthe Rostand wa African Lyon iliyoshuka daraja. Wanaweza kumpa changamoto chanya Agyei na kuiimarisha nafasi hiyo.
Upande wa walinzi , kwanza kabisa ni lazima apatikane mlinzi wa kushoto kumsaidia Zimbwe Jr . Ya Mungu mengi , ipo siku ataumia au kuumwa na kuigharimu timu.
Hamadi Juma beki ya kulia bado si mchezaji makini kwa kiwango alichoonesha kwa msimu huu hususani alipoumia na kulambwa kadi nyekundu Besala Bukungu. Si mzuri katika mifumo ya kutumia walinzi wa pembeni katika kujenga mashambulizi na kuna wakati ana katika kwenye marking. Mnaweza kumtoa kwa mkopo ili kupata beki makini ambaye atakuwa bora kwenye michuano ya kimataifa. Kuna tetesi za kumnyakua Shomari Kapombe wa Azam FC . Ni chagua sahihi . Ni mzoefu na anatosha kwenye patterns zote za kulinda na kushambulia.
Novalt Lufunga sioni mustakabali wake katika kikosi cha ushindani cha 2017-18. Huyu pia anahitajika mbadala wake katika kusuka vyema eneo la walinzi wa kati . Mwanjali licha ya umri lakini bado anawafaa sanjari na Juuko Murshid .
Eneo la kiungo bado Kotei , Mkude , Muzamiru , Shiza , Mohamedi Ibrahimu, na Saidi Ndemla wanafaa kuendelea na timu hiyo lakini Mwinyi Kazimoto na Jamali Mnyate wakaoneshwa mlango wa kutokea . Siwaoni katika hali ya ushindani kuijenga Simba mpya 2017-18 kwa ajili ya ligi na kombe la Shirikisho.
Safu ya ushambuliaji ndio inahitaji marekebisho makubwa. Juma Luizio ambaye mmemchukua kwa mkopo Zesco hana nafasi ya kuendelea na Simba SC msimu ujao . Ni mchezaji wa kiwango cha wastani sana . Goli tatu katika kandarasi ya miezi 7 kwa mshambuliaji ambaye amepata takribani mechi 10 si kiwango kizuri.
Pastory Athanas ulikuwa usajili wa kishabiki na haukuzingatia mahitaji ya Simba SC kimbinu na kiufundi. Atolewe kwa mkopo na kutoa nafasi kwa wazawa wenye uchu na goli kama Mbaraka Abeid toka Kagera Sugar, Abdulrahman Musa wa Ruvu Shooting mfungaji bora msimu huu au Ditram Nchimbi wa Mbeya City ambaye amemaliza mkataba na klabu hiyo.
Blagnon ni wakati wa kuachana nae na kutazama upya anga za kimataifa kupata mshambuliaji makini mwenye uwezo wa kuwapa si chini ya goli 15 kwa msimu na mwenye uwezo na uzoefu wa mechi za kimataifa. Nadhani matazamio makubwa yapo kwa Emanuel Okwi lakini kama mtakuwa na scouting nzuri ni bora mngetafuta ingizo jipya Afrika ya magharibi au Kusini mwa Afrika ambao kwa hakika wana uwezo mzuri kwenye mechi za kimataifa kutokana na vilabu vyao na nchi zao kushiriki mara kwa mara michuano ya CAF kwa mafanikio.
Mavugo bado ni mchezaji mzuri ni kiasi cha kumtafutia kombinesheni nzuri kuanzia eneo la kiungo na pacha wake kwenye ushambuliaji. Anahita mawinga wenye macho mazuri kwenye pasi za chini na juu pia kiungo mchezeshaji mwenye mahesabu mazuri ya pasi zake za mwisho kama alivyo Haruna Niyonzima wa Yanga SC au Rafael Daudi wa Mbeya City. Hapo Mavugo anaweza kurudi kwenye rekodi ya goli zake 30 kwa msimu kwa sababu ana uwezo mzuri kwenye composition yaani jicho nzuri la kucheka na nyavu.
Endapo Yanga SC watashindwa kuendelea na Donald Ngoma ambaye mkataba wake unakwenda ukingoni mwezi ujao , Simba wakimpata mchezaji huyu anaweza kuwasaidia sana . Ngoma ni mzuri sana kucheza kama mshambuliaji namba mbili mchezeshaji hivyo anaweza kuunda pacha makini sana na Mavugo na wakacheka na nyavu watakavyo ligi kuu na Hata michuano ya kombe la Shirikisho.
Mwisho
Poleni sana wana msimbazi wote kwa msiba wa mwanachama wenu mwandamizi mdogo wetu Shose Wazza . Bwana alitoa na Bwana ametwaa jina lake lihimidiwe

No comments:
Write comments