Saturday, 3 June 2017

Tibaijuka ataka Serikali isikilize ushauri wa Lissu kwenye sakata Madini




ALIYEKUWA Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka, ameishauri serikali kuwatumia wataalamu waliopo nchini kutatua changamoto zilizojitokeza kwenye sekta ya madini akiwamo Tundu Lissu, kwa kuwa kuwadharau na kuamua kutowatumia kuna athari kubwa kwa taifa.


Tibaijuka ambaye pia ni Mbunge wa Muleba Kusini (CCM), aliyesema hayo bungeni mjini hapa jana alipokuwa anachangia makadirio ya bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka ujao wa fedha.

Alisema changamoto zinazoikabili sekta ya madini nchini kwa sasa zinaanzia kwenye ardhi na kuonya kuwa kitendo cha serikali kuwadharau wataalamu wa masuala ya mazingira na kuwaona kama wanaharakati, kina athari kubwa kwa taifa.

Alisema Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Mwanasheria Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Mbunge wa Singida Mashariki (Lissu), ni miongoni mwa "vijana" wanaounda Chama cha Wanasheria watetezi wa Mazingira (LEAT) lakini wamekuwa wakichukuliwa kama wanaharakati.

"Tatizo (katika madini) linaanzia kwenye ardhi. 'Section' (Ibara ya) 70 ya Sheria ya Madini inatambua ardhi. Huwezi kuchimba madini kabla ya kuwaondoa wananchi," alisema na kufafanua zaidi:

"Nilipokwenda kule Geita (akiwa waziri), Mheshimiwa (Joseph Kasheku) Musukuma anajua, niliwataka wawekezaji wawalipe wananchi fidia ya ardhi na wakawalipa mambo yakaisha.

"Kikubwa ni majadiliano, wapo vijana wazuri pale LEAT, tuwatumie vizuri kwa manufaa ya taifa. Lissu ni mmoja wa hao wataalamu lakini wanachukuliwa kama wanaharakati. Madhara ya kuwadharau ndiyo haya tunayaona."

Prof. Tibaijuka pia alipongeza Rais John Magufuli kwa kuunda kamati kuchunguza mchanga wa madini akilieleza Bunge kuwa "Rais amesema kile ambacho kilikuwa kinafahamika kwa wengi lakini hawakusema".

Aliwashauri wabunge wenzake kuwa wamoja kusaka mbinu za kulisaidia taifa kunufaika na sekta ya madini badala ya kunyoosheana vidole na kusaka mchawi

No comments:
Write comments