Thursday 9 March 2017

BUNGE LA MALAWI LIKO KTK MCHAKATO WA MABADILIKO,RAIS MUTHARIKA KUHOJIWA


BUNGE la Malawi liko katika mchakato wa mabadiliko ya kanuni zake ili pamoja na mambo mengine, liweze kumwita na kumhoji Rais wa nchi hiyo,Profesa Peter Mutharika, kujibu maswali kadhaa yanayohusu mwenendo wa nchi hiyo pale inapolazimu.
Lakini si tu Mutharika ambaye kwa sasa ndiye yupo madarakani na ni kama vile mabadiliko hayo yanamlenga moja kwa moja, bali hata marais wengine watakaomfuatia baada ya kustaafu kwake, nao pia watalazimika kufika bungeni kwa ajili ya kuhojiwa kwa kadiri Bunge hilo la Malawi litakavyoamua kuhusu kuendelea na kanuni zake hizo mpya.
Mapendekezo ya mabadiliko ya kanuni yamewasilishwa katika Bunge la nchi hiyo na Kamati ya Mambo ya Sheria ya Muhimili huo na katika kanuni husika, itawekwa bayana siku na muda ambao mkuu wa nchi atafika bungeni kwa ajili ya shughuli ya mahojiano.
Katiba ya Malawi chini ya kifungu chake namba 89 (4) inaeleza kwamba rais anapaswa kwenda bungeni kwa ajili ya kipindi cha kujibu maswali ya wabunge tu na sasa kanuni zinarekebishwa ili aweze kuitwa hata nyakati nyingine kwa kadiri masuala mazito ya kitaifa yatakavyokuwa yakijitokeza.
Mwenyekiti wa kamati hiyo ya Bunge, Maxwell Thyolera, amezungumzia hatua hiyo akisema kwamba wamependekeza kanuni mpya ili kumleta rais bungeni kwa ajili ya muda wa maswali siku ya Jumatano na hata ikibidi mara kwa mara kwa kadiri ya makubaliano ya wabunge.
Thyolera alisema rais atatakiwa kujibu si zaidi ya maswali matano katika kila kikao atakachoitwa. “Muda wa kumuuliza maswali rais itakuwa ni saa moja na dakika thelathini,” alisema Thyolera.
“Kuongeza muda wa maswali haitaruhusiwa, kulingana na kanuni namba 68 (kifungu cha 5 na 6). Hata hivyo, maswali matano ya nyongeza katika maswali ya msingi yataruhusiwa lakini hayatatumika katika kujumuisha masuala ambayo hayapo kwenye maswali ya msingi,” alifafanua
Tofauti na kipindi ambacho mawaziri hujibu maswali kutoka kwa wabunge, rais ataheshimiwa na atalindwa, kanuni hiyo mpya imebainisha.
Kwa sasa, kanuni inamruhusu rais aliyeko madarakani kumpa waziri wake yeyote kazi ya kujibu maswali yanayoelekezwa kwake katika siku za Jumatano.
Mutharika amewahi kufanya hivyo mara mbili kwa kiongozi wa Bunge kujibu maswali ambayo mengi yalikuwa yametolewa na kiongozi wa upinzani bungeni Lazarus Chakwera.
Rais wa zamani Bakili Muluzi alikabiliana na kiongozi wa upinzani wa wakati huo, Gwanda Chakuamba, bungeni katika muda uliosisimua katika historia nchini humo miaka ya 1990.

No comments:
Write comments