Magufuli aonya wamiliki wa magazeti, picha ya askari kumtisha Nape kwa bastola yamtia hasira
RAIS
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli, amechukizwa na
mwenendo wa utendaji kazi wa vyombo vya habari hususan magazeti,
akiwaonya wamiliki wa vyombo hivyo vya habari katika hali inayotafsirika
kuwa kulenga “kuwashughulikia”.
Rais Magufuli ametoa onyo hilo katika
mazingira yanayojibainisha kuwa ni kukerwa na ripoti za habari kuhusu
aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye,
katika kurasa za mbele za magazeti ya jana, Machi 24, 2017. Nape
aliondolewa katika uwaziri juzi, Machi 23, 2017 uamuzi uliozua mjadala
mkali, wengi wakimtaja mwanasiasa huyo kijana kama shujaa katika
kusimamia ukweli.
Katika kurasa za mbele za magazeti mengi,
ikiwa ni pamoja na gazeti la Mtanzania na Mwananchi, Nape amepewa
nafasi kubwa zaidi ya kuripotiwa, karibu robo tatu ya kila ukurasa wa
mbele wa magazeti hayo, huku Rais Magufuli akipewa nafasi finyu
iliyopachikwa habari inayomhusu kuzuia makontena ya mchanga wa madini
pamoja na kukamata magari yaliyomo kwenye makontena yaliyoingizwa nchini
kwa taarifa za uongo.
Akizungumza baada ya kuwaapisha mawaziri,
Dk. Harisson Mwakyembe anayekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo na Profesa Palamagamba Kabudi anayekuwa Waziri wa Katiba na
Sheria, Ikulu jijini Dar es Salaam jana, Machi 24, 2017, Rais Magufuli
alisema; “…angalieni wamiliki wa habari.”
Rais Magufuli alionya kwamba vyombo vya
habari katika baadhi ya nchi, akiitaja moja kwa moja Rwanda, vimekuwa
chanzo cha machafuko na kutokana na hali hiyo, akarejea tukio
lililofanywa na mtu anayedhamiwa kuwa askari polisi dhidi ya Nape.
Mtu huyo alichomoa bastola kiunoni mwake
na kumtishia Nape akimuamuru asingumze na waandishi wa habari na badala
yake aingie ndani ya gari na kuondoka. Magazeti yaliyonesha picha ya
askari huyo hatua kwa hatua, namna anavyochomoa bastola na kumuelekezea
Nape, na uamuzi huo wa kitaaluma wa magazeti kupitia wahariri wa
kuchapisha picha hiyo kurasa za mbele, umemkera Magufuli.
Picha hiyo kwa namna fulani inafanana na
ile ya tukio la kuuawa kwa mwanahabari Daudi Mwangosi, ambayo
ilichapishwa katika gazeti la Mwananchi na mpiga picha wake kushinda
tuzo ya mwaka ya mpiga picha bora, kupitia mashindano ya taaluma ya
uandishi wa habari yanayoandaliwa na wadau mbalimbali wa habari, chini
ya uratibu wa Baraza la Habari Tanzania (MCT).
Kutokana na kukerwa huko, Magufuli
alisema namna picha hiyo ilivyochapishwa imetoa ujumbe kuwa ni kama
serikali inaunga mkono tukio hilo. Alimtaka Mwakyembe kwenda kufanya
kazi, kazi ambayo hata hivyo, hakufafanua ni kama inalenga kuminya zaidi
vyombo vya habari ama la.
“Mwakyembe nenda kafanye kazi, tofauti na
wengine ambao walikuwa wakiogopa kuchukua hatua,” aliamuru Rais
Magufuli, katika maelezo ambayo yanaweza kutafsiriwa kumlenga Nape
Nnauye ambaye naye akiwa waziri, alifungia baadhi ya redio na magazeti.
Katika maelezo yake hayo vile vile Rais Magufuli alivitaka vyombo vya
habari kuandika masuala ya maendeleo.
Uamuzi wa kumwondoa Nape katika uwaziri
msingi wake unatajwa kuwa ni tukio la mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam
kuvamia kituo cha televisheni cha Clouds Media Group na kutokana na
tukio hilo, Nape, akiwa waziri anayesimamia tasnia ya habari, aliunda
kamati ya watu watano kuchunguza sakata hilo, kamati hiyo ilimkabidhi
ripoti ambayo naye aliahidi kuiwasilisha kwa mamlaka za juu, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu. Hata
hivyo, siku moja baada ya kupokea ripoti hiyo, Nape aliondolewa kwenye
baraza la mawaziri
No comments:
Write comments