Nape alivyojitabiria kuvuliwa uwaziri wa habari
Mtu anapopatwa na jambo, ni kawaida ya binadamu kuangalia mambo au kauli zake alizokuwa akitoa kabla ya kufikwa na tukio hilo.
Mara nyingi mambo au kauli hizo huonyesha kama vile alikuwa akiona tukio likimjia au kumtokea.
Unaporejea kauli za hivi karibuni za Nape
Nnauye, unaona dhahiri kuwa alikuwa kama anaona kinachokuja na
kujitabiria kuwa angevuliwa uwaziri wa habari, utamaduni, sanaa na
michezo.
Kauli ya mwisho na yenye nguvu aliitoa
juzi mchana wakati wa mkutano na waandishi wa habari wa kukabidhiwa
ripoti ya uchunguzi kuhusu tukio la uvamizi wa studio za televisheni za
kampuni ya Clouds Media Group.
“Niseme tu kwamba nimepokea ripoti na
kama nilivyosema kazi hii si rahisi sana, ina gharama kubwa sana.
Gharama ya kusimamia haki, kusimamia ukweli,” alisema juzi.
Kauli hiyo aliirudia jana wakati akiongea
na waandishi wa habari nje ya Hoteli ya Protea baada ya kuzuiwa kufanya
mkutano wake ndani.
Nape aliondolewa katika nafasi hiyo
katika mabadiliko madogo yaliyofanyika jana asubuhi, siku moja baada ya
kukabidhiwa ripoti hiyo ambayo aliahidi angeiwasilisha kwa mamlaka za
juu, ambazo alizitaja kuwa ni Waziri Mkuu, Makamu wa Rais na Rais.
Katika mabadiliko hayo, Rais Magufuli
amemteua Profesa Palamagamba Kabudi kuwa Waziri wa Katiba na Sheria,
nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na Dk Harrison Mwakyembe ambaye anaziba
nafasi ya Nape.
Ni kama Nape alikuwa akiona gharama za
kusimamia haki za Clouds Media za kutoingiliwa katika shughuli zake na
viongozi baada ya kituo hicho kuvamiwa na askari waliokuwa na silaha za
moto wakimsindikiza kiongozi aliyekwenda kuhoji sababu za kituo hicho
kutorusha habari ya ‘umbea’ iliyokosa sifa stahiki.
Maneno hayo ya Nape ni sehemu ya mlolongo
wa kauli za utabiri ambazo amekuwa akizitoa kwa siku chache zilizopita
wakati akizungumza na waandishi na kwenye mitandao ya kijamii.
Baada ya kituo cha Clouds kuvamiwa, Nape
alituma ujumbe kwenye akaunti yake ya Tweeter Machi 20 akisema “No
Longer at Ease”, ikiwa ni nukuu ya kitabu cha fasihi kilichoandikwa na
Chinua Achebe mwaka 1960 kumaanisha hakuna marefu yasiyokuwa na mwisho.
Siku hiyo, Nape alituma ujumbe mwingine
katika akaunti hiyo akisema “each day is a day of decisions, and our
decisions determin our destiny” akimaanisha “kila siku ni siku ya uamuzi
na uamuzi wetu huamua mustakabali wetu”.
Kama vile haitoshi, Nape alituma ujumbe
mwingine siku hiyo akisema “majaribu huja ili kutuinua kutoka utukufu
hadi utukufu. Kikubwa tusikate tamaa, utukufu mkubwa upo mbele. Quaresma
njema”.
Nape aliandika hayo wakati mchakato wa kamati aliyoiunda ikiendelea kuchunguza tukio la Clouds kuvamiwa.
Na alikuwa na ushauri kwa wanasiasa
wengine. “Na kwa kuwa sisi wengine tuliopewa dhamana ya kuwatumikia watu
ni vizuri kujifunza kuwa wanyenyekevu, kwanza ina baraka kwa Mwenyezi
Mungu, lakini pia tutakuwa tunawatendea haki Watanzania ambao ndiyo
wametuchagua na kutuweka kwenye madaraka.”
Baada ya kuvuliwa uwaziri, Nape jana
alituma tena ujumbe katika akaunti yake ya Tweeter akiandika kwa herufi
kubwa baadhi ya maneno kuweka msisitizo.
“Ndugu zangu naomba TUTULIE! LEO (jana)
mchana nitakutana na wanahabari na tutalizungumza hili. Nitawaambia saa
na mahali. Kwa sasa naomba TUTULIE!”
Baadaye akatuma ujumbe mwingine akisema
“tukutane saa nane kamili Protea Hotel karibu na St. Peter. Nitakutana
na wanahabari. Karibuni sana!”
Kauli za wadau
Wadau wa habari wakiwamo wanasiasa,
wasomi, wachambuzi wa masuala ya kisiasa na wanahabari wameeleza
kushtushwa na mabadiliko hayo na kummimia sifa mbunge huyo wa Mtama.
Katibu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania
(TEF), Nevile Meena alisema tasnia ya habari imepokea kwa huzuni taarifa
hiyo, hasa kutokana na ukweli kuwa ameondoka katika kipindi ambacho
alikuwa karibu na wadau akitetea uhuru wa habari.
“Tulitegemea Nape angeondoka wizara hiyo,
lakini hatukutegemea ingekuwa kwa mtindo huu. Katika sakata hili Nape
alionyesha wazi kutoegemea upande wa Serikali na alisimamia haki,”
alisema Meena.
Kuhusu nafasi hiyo kuchukuliwa na Dk
Mwakyembe, Meena alisema tasnia inamkaribisha, ikitegemea atafanya
vizuri, “asipokwenda sawa tutaenda naye hivyohivyo”.
Kauli ya masikitiko pia ilitolewa na
Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari (UTPC) ambayo rais wake,
Deogratius Nsokolo alisema, “Nape alikuwa karibu mno na waandishi na
wadau wote wa habari na alikuwa akisimamia haki”.
Alisema huenda kilichomgharimu Nape ni kwenda kutembelea kituo cha Clouds na kuunda kamati ya kuchunguza uvamizi huo.
“Nimsihi Nape asikate tamaa. Yeye ni
mwanasiasa mzuri na mkomavu. Hakuna ubishi tena, ni shujaa ambaye
amejitoa kusimamia haki. Sina uhakika sana kama atakayeshika nafasi yake
atakuwa kama yeye,” alisema.
Wanasiasa
Akizungumzia kuondoka kwa Nape, Mbunge wa
Kigoma Mjini, Zitto Kabwe alisema haitoshi kumlilia Nape, bali wananchi
wanapaswa kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria.
“Haifai tu kumlilia Nape kwamba anaonewa,
tunapaswa kumuwajibisha Rais ambaye amechaguliwa na wananchi. Anapaswa
kuwa mnyenyekevu kwa wananchi na hatupaswi kuendekeza tabia zozote za
utawala wa kiimla,” alisema kiongozi huyo wa ACT Wazalendo.
“Ni lazima sisi viongozi tuwaelekeze wananchi mabaya au mazuri na tuwaelekeze kuchukua hatua.”
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe
alisema kilichotokea ni uthibitisho wa madai ya muda mrefu ya wapinzani
kuwa Rais Magufuli anapingana na mawazo ya wananchi wake.
“Huu ni uthibitisho kuwa tuna Rais ambaye
anapingana na maoni ya watu anaowaongoza. Kinachoendelea hapa si Rais
au Nape, bali ni hisia za wananchi. Nape amejipambanua hivi karibuni
kama waziri makini na alichokifanya kiko ndani ya uwezo wake,” alisema
Mbowe.
“Sisi kama wapinzani tunaona tunashamiri
kwa sababu CCM inasambaratika, lakini si jambo la kufurahi tu, bali
tuisaidie nchi yetu.
“Kitu cha msingi Rais anapaswa kuwa
mwepesi wa kusikiliza kuliko kuongea. Marais wengi wamefanikiwa kwa
kusikiliza wananchi wao, lakini Rais Magufuli ni tofauti, anaongea
kuliko kusikiliza maoni ya wananchi wake. Ndiyo maana mawaziri
wanajiuzulu, wabunge wanajiuzulu kwenye kamati zao, yote kwa sababu Rais
hataki kusikiliza maoni yao,” alidai Mbowe.
Lakini Mkurugenzi wa Taasisi ya
Demokrasia na Utawala Bora (Fordia), Bubelwa Kaiza aliunga mkono hatua
ya Rais Magufuli akisema kuwa aliitarajia.
“Binafsi hatua hii niliitegemea kwa
sababu vitendo alivyovifanya Nape ni kama hakujua kuwa Serikali ndiyo
inayojisimamia. Alipaswa kuomba ushauri kabla ya kuunda ile kamati
yake,” alisema Kaiza.
“Ni kweli kama Waziri wa Habari
angekwenda kutembelea Clouds Media, lakini asingesema chochote. Lakini
yeye aliunda kamati na kufanya aliyofanya jana (juzi). Kwa Serikali
iliyo makini ni lazima izibe vaccum (ombwe) inayojitokeza.”
Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya
Mwananchi Communications Limited (MCL), Francis Nanai alisema kama
wamiliki wa vyombo vya habari wako tayari kufanya kazi na waziri yeyote
anayeteuliwa na Rais, ilimradi tu afuate misingi na weledi wa kazi hiyo.
“Kitakachotukosanisha naye ni kama atakandamiza uhuru wa habari,” alisema Nanai.
“Tunampongeza waziri mpya, Dk Harrison
Mwakyembe kwa kuteuliwa na pia tunampongeza Nape Nnauye anayeondoka kwa
kazi kubwa aliyoifanya. Kuondoka kwake kumetushtua kwa sababu tulikuwa
naye kwenye kazi na sasa itabidi tuanze na mtu mpya.”
Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi alisema Nape ameondoka kishujaa kwa sababu alikuwa amebeba matumaini ya Taifa.
Alisema kutokana na kuondoka kishujaa,
anayo nafasi ya kuteuliwa tena kuongoza wizara nyingine na alimsifu kwa
jinsi alivyosimamia suala la kuvamiwa kwa studio za Clouds Media.
Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Mohamed Bakari alisema kitendo cha
kuondolewa kwa Nape saa chache baada ya kupokea ripoti, kinaashiria kuwa
Rais John Magufuli hapendi kushauriwa.
“Waziri aliyewekwa, Dk Harrison Mwakyembe
ameonyesha kutosimamia mambo yake katika wizara alizotoka. Hana
msimamo,” alisema Dk Bakari na kuongeza kuwa ni mapema kumzungumzia
waziri mpya wa Katiba, Profesa Kabudi kwa kuwa ndio kwanza ameteuliwa.
Askofu Gwajima
Askofu Josephat Gwajima, ambaye alisema
habari iliyomtuhumu kuwa amezaa na mwanamke mmoja wa jijini Dar es
Salaam ndiyo iliyosababisha Clouds kuvamiwa, jana pia alijibebesha mzigo
wa Nape.
Akiwa katika ziara ya kituo cha redio cha
EFM, Askofu Gwajima alisema: “Sababu zilizofanya Nape aenguliwe
zinanihusu sana mimi, sababu mkuu wa mkoa alivamia mahali kuwalazimisha
warushe kipindi kinachonihusu. “Nataka kila mtu ajiulize je, ni nani
aliyekwenda kushinikiza Clouds kwamba material (kipindi) za kumchafua
Askofu Gwajima zipigwe, ni nani? Nani alikuwa nyuma ya Mkuu wa Mkoa hata
kiasi kwamba Nape aondolewe uwaziri?”
Wanamuziki wazungumza
Nape pia alikuwa anaongoza wizara inayowahusu wasanii, ambao pia wameeleza kushtushwa.
“Nape endelea kuwa mwerevu,” alisema mwanamuziki wa miondoko ya Bongo Fleva, Nick wa Pili alipozungumza na gazeti hili.
Nick alisema inauma ingawa haijulikani
kwa nini amebadilishwa na kuwekwa mwingine, lakini kitendo cha
kuondolewa kwake ni pengo kwa wasanii kwa sababu alikuwa ni mtu
anayepatikana kirahisi.
“Tusubiri tuone huyu mpya itakuwaje. Inawezekana akaendeleza mazuri tuliyoanza Nape,” alisema Nick wa Pili.
Rais wa Mfuko wa Muziki Tanzania, Dk Donald Kisanga alimtaka Nape kusonga mbele.
“Mapambano bado yanaendelea. Wewe bado kijana tena jasiri, bado una fursa ya kufanya vitu vingi zaidi,” alisema.
Alisema kinachosikitisha ni kuondolewa
kwenye nafasi aliyopo kwa sababu alionekana kuimudu, ingawa matumaini
yapo pia kwa anayekuja.
Muigizaji aliyebobea, Dk Cheni alisema hakuna anayefahamu Rais anawaza nini, hivyo ni vyema kusubiri kitakachotokea.
Mwigizaji mwingine wa filamu, Johari
Chagula alisema uamuzi huo umemuuma kwa sababu Nape alikuwa waziri pekee
aliyejitokeza hadharani na kupigana vita moja, akisikiliza matatizo ya
wasanii bila kupitia mtu mwingine.
“Kiukweli alitutoa eneo moja kutupeleka jingine. Alikuwa amesimama katikati ya masilahi yetu,” alisema Johari.
Mstuko kwa wanamichezo
Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Wavu
Tanzania (Tava), Agapa Agostino alisema ni mapema Nape kuondolewa kwa
kuwa tayari alikuwa na mikakati mingi katika kuboresha tasnia ambayo
ameiachia njiani.
“Naheshimu uteuzi wa Rais. Ni maamuzi
yake, lakini naona kama imekuwa mapema mno Nape kuondolewa. Pamoja na
yote, namshauri mrithi wake kuendeleza mipango yote mizuri iliyoachwa na
Nape na mabaya kuyaweka kando,” alisema.
Kocha wa judo, Zaid Hamis alisema
misimamo ya Nape katika kutetea masuala ya habari ndiyo imechangia
kuenguliwa katika nafasi hiyo.
Katibu Mkuu wa Chama cha Riadha Arusha,
Alfredo Shahanga alisema mwenye uamuzi ni Rais, na kwamba watafanya kazi
na yeyote yule watakayeletewa.
“Rais ndiye mwenye mamlaka ya kuteua
mawaziri hivyo maadamu kaona inafaa Nape aondoke ni sawa na sisi
tutafanya kazi na waziri yeyote tutakayeletewa,” alisema
No comments:
Write comments