Thursday, 16 March 2017

Mugabe Afuja Mabilioni ya Pesa Kukodi Ndege ya Kifahari Huku Nchi Yake Ikinuka Umasikini

RAIS Robert Mugabe wa Zimbabwe mwishoni mwa wiki iliyopita amefuja zaidi ya dola milioni moja za Marekani kwa ajili ya kukodi ndege ya kifahari Boeing 767-200 aliyoitumia kusafari katika nchi za Singapore na Ghana ilihali nchi yake ikikabiliwa na uchumi mgumu kupindukia.
Hali ya kiuchumi nchini Zimbabwe inaripotiwa kuwa mbaya kiasi kwamba imekuwa vigumu kulipa hata mishahara ya watumishi wa serikali.
Kwa mujibu wa Jarida la Indipendent, uchunguzi unabainisha kwamba ndege hiyo aliyotumia Rais Mugabe, 767 Boeing Business Jet (BBJ) yenye usajili P4-CLA, kuanzia Machi Mosi hadi Machi 6, mwaka huu, ilifanyiwa malipo katika kampuni yake ya zaidi ya dola za Marekani milioni moja. Ndege hiyo inaendeshwa na Kampuni ya Comlux Aviation, yenye ofisi zake Bahrain.
Inaelezwa kwamba ndege hiyo ya kifahari inavyo vyumba vya faragha, ofisi kubwa sambamba na muundo wa kuvutia ndani unaonakshiwa na vifaa vya kisasa.
Taarifa hizi za Mugabe kukodi ndege ya kifahari kwa fedha nyingi zinajitokeza huku tayari kukiwa kumeripotiwa taarifa nyingine zinazobainisha kwamba kiongozi huyo huyo amekuwa na matumizi ya ufujaji wa fedha katika usafiri.
Inadaiwa kwamba safari zake za ndani na nje ya nchi zimepata kutumia takriban dola za Marekani milioni 36 katika miezi 10 ya mwanzo ya mwaka 2016 katika nchi ambayo sekta ya afya imekuwa ikikabiliwa na uhaba mkubwa wa dawa, zikiwamo hata dawa za kutuliza maumivu katika hospitali za umma.
Kwa mujibu wa vyanzo vya habari vya Jarida la Independent, Mugabe amelazimika kukodi ndege hiyo ya kifahari baada ya ndege yake ambayo amekuwa akiitumia kwa safari zake ya Shirika la Ndege la Zimbabwe (AirZim) kuhitaji matengenezo makubwa kabla ya kuruka safari za masafa marefu.
Hata hivyo, hali hiyo ya Shirika la Ndege la Zimbabwe kushindwa kuifanyia matengenezo ndege hiyo kutokana na ukata inamweka katika wakati mgumu mkwe wa Rais huyo wa Zimbabwe, Simba Chikore, ambaye ndiye bosi mkuu wa operesheni katika shirika hilo la ndege la taifa.
AirZim, ambalo wakati Zimbabwe inapata uhuru mwaka 1980 chini ya Robert Mugabe lilikuwa na jumla ya ndege 18 zilizokuwa zikifanya kazi, kwa sasa shirika hilo limekuwa na jumla ya ndege nne tu zinazofanya kazi ambazo ni Airbus A320, Boeing 767 na nyingine 737 pamoja na MA60 kutoka China.
“Shirika la Ndege la Zimbabwe limeshindwa kuifanyia matengenezo yanayohitajika ndege ya Rais Mugabe kwa kuwa wakala wake wa vifaa bado hajalipwa deni lake la awali,” kilieleza chanzo cha habari cha Independent na kuongeza kuwa: “..shirika kwa sasa limekuwa katika hali mbaya.”
Waziri wa Usafiri wa Zimbabwe, Joram Gumbo, aliliambia gazeti la Independent mwishoni mwa wiki hii kwamba wizara yake imechukua uamuzi wa kukodi ndege hiyo kwa kuwa ile inayotumiwa na Mugabe ya Shirika la Ndege Zimbabwe ni mbovu.
“Tumelazimika kukodi ndege kutoka Bahrain kwa sababu ile ndege inayotumiwa na rais inaendelea kufanyiwa matengenezo. Hivi tunavyozungumza tayari vifaa kwa ajili ya matengenezo vimekwishaletwa na muda si mrefu itakuwa hewani ikiendelea na shughuli, lakini rais asingeweza kusubiri hadi matengenezo yakamilike ilipaswa aendelee na ratiba yake,” alisema Gumbo na kuongeza; “Tulifanya jitihada za kutafuta ndege ya kukodi katika ukanda wetu wa Afrika. Afrika Kusini nao wamekuwa na matatizo yao kama ilivyo kwa Angola. Kukodi ndege kwa ajili ya rais si jambo jipya na la ajabu, rais ndiye mteja namba moja wa shirika letu.”
Kwa mujibu wa Gumbo, gharama za kukodi ndege hiyo ni za kawaida na kwamba tofauti kubwa ya bei imetokana na ukweli kwamba ndege hiyo imesafiri kutoka mbali.
Mugabe mwenye umri wa miaka 93, amesafiri kwenda Singapore kwa ajili ya kutazamwa afya yake katika moja ya hospitali zenye gharama za juu kabisa za matibabu nchini humo ya Gleneagles. Baada ya hapo, Mugabe atasafiri kuelekea Ghana ambako atakuwa na ziara nchini humo.
Kwa mujibu wa tovuti ya Kampuni ya Ndege ya Comlux, ndege ya aina hiyo, yaani Boeing 767 BBJ imetengenezwa kwa ajili ya kutumiwa na marais wa nchi mbalimbali, familia za kifalme na watu wengine mashuhuri katika tasnia ya biashara duniani, ni ndege ya kifahari yenye uwezo wa kuchukua abiria 63 ikisafiri kwa muda wa saa zaidi ya 14 angani bila kutua.
Uchunguzi zaidi wa gazeti la Independent unabainisha kwamba fedha zilizotumika kukodi ndege hiyo zinajumuisha huduma zote zikiwamo za chakula na vinywaji vya aina mbalimbali ikiwamo mvinyo, huduma ya simu kwa njia ya Satellite na bima ya usalama.
“Kwa namna ndege hii ilivyo, inaonekana kuirusha kwa saa moja angani inatumia dola za Marekani takriban 9,138,” anaeleza mtaalamu mmoja wa masuala ya anga.
Katika miezi sita ya kwanza ya mwaka 2016, Mugabe alisafiri umbali wa kilomita 200,000 angani. Akiwa amesafiri kwenda nchini Singapore zaidi ya mara 10 katika mwaka huo wa 2016.

No comments:
Write comments