Saturday, 4 March 2017

RAIS MAGUFULI AITAKA TPA KUZUIA MIANYA YA UPOTEVU WA FEDHA ZA UMMA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, ameitaka Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kuachana na utaratibu wa kutoa zabuni za uendeshaji wa bandari kwa kampuni binafsi ambazo huingia mikataba isiyo na manufaa kwa nchi na kusababisha uwepo mianya ya upotevu wa fedha za umma.

Mhe. Rais Magufuli ametoa agizo hilo jana  tarehe 04 Machi, 2017 muda mfupi kabla ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa gati namba 2 ya bandari ya Mtwara ambayo ujenzi wake unatarajiwa kuchukua muda wa miezi 21 kuanzia sasa.

“Kwa sababu mmeamua kuichimba hii bandari ili kuongeza kina mpaka mita 15 kwa kutumia fedha zetu, sitegemei TPA na Wizara kuingia tena mkataba na wawekezaji wengine, kwa sababu imekuwa ni kawaida hapa Tanzania, tunatumia fedha zetu halafu wanakuja watu wengine kufanya biashara na fedha zetu kana kwamba nchi hii haina wasomi, na wanaokuja kuendesha kweli wanaiba” alisema Mhe. Rais Magufuli.

Mapema Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa alisema gati namba 2 itakayojengwa katika bandari ya Mtwara itakuwa na urefu wa mita 350 na ujenzi wake utagharimu Shilingi Bilioni 137.5 zote zikiwa zimetolewa na Serikali ya Tanzania.

Nae Mkurugenzi Mkuu wa TPA Mhandisi Deusdedit Kakoko alisema imelazimu kuongeza gati katika bandari ya Mtwara baada ya kuwepo ongezeko la mizigo inayosafirishwa kupitia bandari hiyo ambapo kiwango cha mizigo inayohudumiwa kinatarajiwa kuongezeka kutoka tani 273,886 mwaka 2015/2016 hadi kufikia tani 388,000 mwaka 2016/2017 kiwango ambacho kinakaribia ukomo wa uwezo wa bandari hiyo yenye uwezo wa kuhudumia tani 400,000 kwa mwaka.

Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amefungua Kituo cha Biashara cha Benki ya NMB Mjini Mtwara na kutoa maagizo kwa Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango kutoa maelekezo ili fedha zote za Serikali zipitie Benki ya NMB ambayo licha ya hisa zake kumilikiwa na Serikali kwa asilimia 32 imekuwa ikitoa gawio kwa Serikali kila mwaka ambapo mwaka 2016 ilitoa Shilingi Bilioni 16.5 na mwaka huu inatarajia kutoa zaidi ya kiwango hicho cha gawio.

“Na nikuombe Waziri, kwa sababu wewe ndio unayesimamia fedha za Serikali, toa maelekezo ili fedha zote zipitie benki ya NMB, labda kama kutakuwa na umuhimu sana wa kupitia benki nyingine” alisema Mhe. Rais Magufuli.

Mhe. Rais Magufuli ambaye ameipongeza benki ya NMB kwa kujikita kutoa huduma za kibenki kwa wananchi wa kawaida na wafanyakazi nchi nzima ametoa wito kwa benki zote nchi kupunguza viwango vya riba ili Watanzania wengi waweze kukopa na kufanya shughuli za uzalishaji mali.

Katika hatua nyingine, Mhe. Rais Magufuli amefungua jengo la Benki Kuu ya Tanzania (BOT) Mjini Mtwara ambalo limejengwa kwa gharama ya Shilingi Bilioni 31 na linatoa huduma za Benki Kuu katika kanda ya kusini inayojumuisha Mikoa ya Mtwara, Lindi na sehemu za Mikoa ya Pwani na Ruvuma.

Pamoja na kumpongeza Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuridhia ujenzi wa jengo hilo na kuipongeza BOT kwa kufanikisha ujenzi huo na kusimamia vizuri uchumi wa nchi, Mhe. Rais Magufuli ameitaka benki hiyo kuu kuchukua hatua kali dhidi ya benki ambazo zimekuwa zikikiuka maadili na taratibu za kibenki ikiwemo kushiriki njama za kuiba fedha za Serikali kupitia mikopo na utakatishaji wa fedha.

Aidha, amemtaka Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania Prof. Benno Ndulu aandae utaratibu utakaozibana benki zinazofanya biashara hapa nchini ili zilazimike kuwakopesha wananchi, kupunguza viwango vya riba na kuendeleza shughuli za uzalishaji mali.

Mhe. Rais Magufuli pia amefungua nyumba 40 za makazi za Rahaleo zilizojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Mjini Mtwara kwa gharama ya Shilingi Bilioni 10.5 na ameipongeza NHC kwa kazi nzuri ya ujenzi wa nyumba za makazi ya wananchi katika maeneo mbalimbali nchini.

Akiwa katika mradi huu Mhe. Dkt. Magufuli ameagiza kuanzia sasa Mkoa, Wilaya ama Kiongozi yeyote atakayeomba kujengewa makazi na NHC ahakikishe eneo lililoandaliwa kwa ajili ya kujengwa makazi hayo linafikishiwa barabara, umeme na maji na ameitaka NHC kuacha kutumia wakandarasi katika ujenzi wa majengo yake na badala yake waunde vikosi kazi vya ujenzi kwa kutumia wataalamu waliopo ndani ya nchi ili kuzalisha ajira zaidi na kupunguza gharama za ujenzi wa majengo.

Mhe. Dkt. Magufuli ambaye jana ameingia Mkoani Mtwara akitokea Mkoani Lindi alisimamishwa na wananchi wa Kijiji cha Mnolela Kilichopo Lindi Vijijini ambapo baada ya kupokea kero ya Kijiji hicho kushindwa kumalizia jengo la zahanati aliamua kulikagua na kisha akatoa mchango wa Shilingi Milioni 15, zitakazojumlishwa na Shilingi Milioni 10 zitakazotolewa na Mbunge wa Jimbo la Mtama Mhe. Nape Nnauye na Shilingi Milioni 30 zitakazotolewa na Halmashauri ya Wilaya ya Lindi Vijijini, na ameagiza ujenzi huo ukamilike ndani ya miezi 3 kuanzia sasa.

Halikadhalika, Mhe. Rais Magufuli alisimamishwa na kuzungumza na wananchi wa Kijiji cha Madangwa kilichopo Lindi Vijijini ambapo baada ya kupokea kero ya ubadhirifu wa fedha za wakulima wa Korosho ameuagiza uongozi wa Mkoa wa Lindi kuwasaka viongozi wote wa vyama vya ushirika wanaotuhumiwa kula fedha za wakulima na kuwachukulia hatua za kisheria.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Mtwara

No comments:
Write comments