RAIS wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein, amesema hakuna mabadiliko yoyote yatakayotokea Zanzibar kama inavyoelezwa na Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad.
Akizungumza na waandishi wa habari Ikulu jana kuadhimisha mwaka mmoja wa uongozi wake wa muhula wa pili, alisema mabadiliko hayawezi kutokea bila kufanyika kwa uchaguzi au mapinduzi.
Alisema ni vyema Maalim Seif awaeleze wananchi na wafuasi wake mabadiliko hayo yatakuja kwa njia gani wakati uchaguzi umeshafanyika na yeye ndiye aliyechaguliwa na wananchi na kushinda kwa asilimia 91.4 katika uchaguzi wa marudio wa Machi 20, 2016, baada ya uchaguzi wa Oktoba 25, 2015 kufutwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).
“Kama Maalim Seif anasema mabadiliko yanakuja, mimi siwezi kumzuia kusema hivyo mwache aseme maana mdomo ni nyumba ya maneno, lakini mimi nasema mabadiliko hayaji ng’oo, mimi ndiye rais wa Zanzibar hadi mwaka 2020, baada ya tume ya uchaguzi kutangaza uchaguzi mwingine,” alisema Dk. Shein.
Alisema hakuna njia ya kupata serikali kama sio kufanyika uchaguzi au kufanyika kwa mapinduzi, hivyo anayesema atapewa serikali bila uchaguzi na kushinda ni kujidanganya.
“Mwenye ubavu wa kiniondoa madarakani mimi nasema aje kuniondoa, hivyo wanaosema huko waache waseme ilimradi hawavunji sheria wala kuibugudhi serikali kupita kiasi.”
Dk. Shein alihoji kuwa huyo anayedai kuwa atapewa serikali atapewa na nani na kwa njia ipi na nani ambaye atamuapisha na kusisitiza kuwa maneno yanayosemwa hayamkoseshi usingizi kwani urais amepewa na wananchi kwa kupigiwa kura.
Aidha, Dk. Shein alisema katika awamu yake ya kwanza ya uongozi ambayo aliongoza serikali ya umoja wa kitaifa akishirikiana na CUF, hakukuwa na mivutano mikubwa kati yake na mawaziri kutoka CUF pamoja na Maalim Seif ambaye alikuwa Makamu wa Kwanza wa Rais, ingawa ziliibuka tofauti wakati serikali hiyo ikimaliza muda wake.
Alisema tofauti hizo zilianza Mawaziri na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wa CUF walipotoka nje ya vikao vya baraza hilo wakati baraza likijadili bajeti ya serikali ya 2015/2016, kutokana na wajumbe wa CUF kutokubaliana na hoja.
“Hapo ndipo tulipoanza kuvutana, lakini mwanzoni mwa muhula wangu wa kwanza wa uongozi tulikuwa tukienda vizuri, tukizungumza, tukicheka na kufurahi na hata tulikuwa tukikaa pamoja kula chakula cha mchana,” alisema Dk. Shein.
No comments:
Write comments