Licha ya ukweli kwamba wajumbe
watatu wa Kamati Kuu ya CCM walitoka nje kujitenga na uamuzi wa chombo
hicho, Sophia Simba ndiye anayeangaliwa zaidi baada ya Halmashauri Kuu
ya chama hicho kuamua kumvua uanachama tofauti na wenzake.
Emmanuel Nchimbi, ambaye sasa ni balozi wa
Tanzania nchini Brazil, amepewa onyo kali, wakati mjumbe mwingine wa
Kamati Kuu, Adam Kimbisa amesamehewa.
Simba, mwanasiasa mkongwe aliyekuwa
mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT) na ambaye amewahi kuongoza wizara
mbili tofauti, anaingia kwenye orodha ya vigogo wa juu wa CCM waliowahi
kuvuliwa uanachama kwa tuhuma tofauti.
Wengine ni Maalim Seif Sharif, Katibu mkuu
wa CUF ambaye alikuwa mwanzilishi wa kikundi cha kupambania demokrasia
cha Kamahuru ambacho baadaye kiliunganishwa na chama cha Civic United
Front (CUF) ambacho kimejijenga kama chama kikuu cha upinzani visiwani
Zanzibar.
Kada mwingine ni Shaaban Mloo ambaye
alifukuzwa CCM mwaka 1988 wakati hali ya kisiasa ilipochafuka Zanzibar.
Kama ilivyokuwa kwa Maalim Seif, baadaye Mloo alijiunga na chama kipya
cha upinzani kilichoitwa Kamahuru.
Mansoor Yusuf Himid ni kigogo mwingine
aliyevuliwa uanachama wa CCM kutokana na misimamo yake. Mansoor, ambaye
alikuwa mwakilishi wa Kiembesamaki, pia aliwahi kuwa mweka hazina wa
CCM-Zanzibar na Waziri wa Maji, Ujenzi, Nishati na Ardhi wakati wa
Serikali ya Dk Amani Karume na Dk Ali Mohamed Shein kabla ya kutimuliwa.
No comments:
Write comments