Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu
imemwonya na kumwambia Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema), kwamba
kadi za onyo kwa ajili yake zimeisha kutokana na kushindwa kuhudhuria
mahakamani siku ya kesi.
Kauli hiyo ilitolewa jana mbele ya Hakimu
Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi baada ya kubaini kwamba ilitolewa hati ya
kumkamata mbunge huyo kwa kushindwa kufika mahakamani.
Halima Mdee alipotakiwa kujitetea aliinuka
na kujieleza kuwa amefika mahakamani hapo akiwa na nyaraka za safari
ikiwamo tiketi na VISA na kwamba taarifa za safari alimpa wakili.
Kwa upande wa wakili wao, Hekima Mwesiga
aliieleza mahakama kuwa nyaraka za kuiarifu mahakama juu ya safari ya
Halima Mdee nje ya nchi kwa bahati mbaya hakuziwasilisha, alikuwa nazo
Peter Kibatala ambaye alikuwa akiendesha kesi ya Mbunge wa Singida
Mashariki, Tundu Lissu.
“Tutaonana wabaya katika hili ni lazima
unapofanya kitu adabu yake ifuatwe, Wakili hakufuata taratibu na Halima
kabla ya kusafiri ulipaswa kutoa taarifa mahakamani ili uweze kupata
ruhusa ya mahakama lakini haukufanya hivyo.
“Sasa nafikiri wote tufuate taratibu za
kuhudhuria mahakamani, Halima Mdee kadi zako za kukuonya zimeisha
tafadhali,”alisema Hakimu.
Mdee na wabunge wengine wa Chadema, Mwita
Waitara, Saed Kubenea na makada wao wanatuhumiwa kumjeruhi Katibu Tawala
wa Mkoa wa Dar es Salaam, Theresa Mmbando.
Kabla ya onyo hilo, mahakama ilisikiliza
ushahidi wa upande wa mashtaka uliotolewa na Mrakibu wa Polisi, ambaye
pia ni Msaidizi wa Operesheni Ilala, Eugen Mwampondele.
Mwampondele alidai siku ya tukio alimwona Rafii Juma na Halima Mdee wakimkunja Theresa Mmbando ili awape nyaraka.
Shahidi huyo alidai waliompiga Mmbando
hawapo mahakamani. Washtakiwa katika kesi hiyo ni Mbunge wa Jimbo la
Ubungo, Saed Kubenea, Diwani wa Kata ya Kimanga, Manase Njema (56),
Halima Mdee (37) na Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara (40).
Wengine ni mfanyabiashara na kada wa chama hicho, Rafii Juma (21)pamoja na Diwani wa Kata ya Saranga, Ephreim Kinyafu (33).
Inadiwa kuwa Februari 27, 2016 katika
Ukumbi wa Karimjee Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam watu hao
walimjeruhi Theresia na kumsababishia majeraha mwilini wakati wa
uchaguzi wa Meya wa Jiji la Dar es Salaam
No comments:
Write comments