Saturday 18 March 2017

WACHEZAJI SIMBA WAMUUMIZA KICHWA OMOG


Juuko_1Leo Jumamosi, Simba na timu ya Madini ya Arusha zinatarajiwa kumenyana katika dimba la Sheikh Amri Abeid kuwania tiketi ya kycheza nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Tanzania Bara.
Wakati mashabiki wengi wakiwaza ushindi, benchi la ufundi la Simba chini ya kocha mkuu Joseph Omog litakuwa linaanza kuumiza kichwa nani anastahili sahihi kuanza katika safu ya ulinzi ya timu kati ya Abdi Banda na Juuko Murshid aliyerejea kikosini hivi karibuni.
Katika pambano la leo, kwa kuwa Method Mwanjale hajawawa fiti kuna uwezekano mkubwa kwa Omog kuamua kuijaribu pacha ya Banda na Juuko.
Mwanzoni mwa msimu huu walinzi hao wa kati hawakuwa na nafasi ya kuanza lakini mambo yakabadilika mechi zilivyozidi kuchezwa. Awali Mwanjale na Lufunga walikuwa wakipewa nafasi kama mabeki wa katikati.
Juuko akampindua Lufunga na kucheza sambamba na Mwanjale hadi alipoenda kwenye Fainali za Kombe la Mataifa Afrika. Banda akaonekana kufaidika na kukosekana kwa Juuko kwa kupewa nafasi ya kucheza sambamba na Mwanjale. Amecheza vizuri kiasi cha kurudishwa timu ya taifa Tanzania.




Wote ni mabeki wazuri wenye sifa ya kukaba kwa kutumia nguvu lakini wanatofautiana kidogo. Juuko ni mzoefu zaidi akiwa mmoja wa wchezaji tegemeo wa timu ya taifa ya Uganda.
Kwa upande mwingine, Banda ana faida ya kucheza nafasi nyingi zaidi ndio maana kwa sababu pembeni kuna Bokungu na kati kuna Mkude na Kotei analajikuta akiwania kucheza katikati.
Mtindo wa kukaba kwa nguvu na kuonesha moyo wa kupambana mbele ya washambuliaji wababe na ‘wajanja wajanja’ kama Donald Ngoma Amissi Tambwe imewajengea kupendwa mno na mashabiki wa Simba kiasi kuwa itapofika wakati kuwa mmoja wao pekee kustahili kuanza sambamba na Mwanjale wengi hupata mchanganyiko wa huzuni na furaha.
Kwa mashabiki wanaoamini falsafa ya kuwa beki hatakiwi kuwa muungwana mbele ya washambuliaji, huwaambii kitu kwa Juuko na Banda ambao ni waumini wa kweli wa falsafa hii.
Msimu uliopita Banda aliamua kujilipua kwa kumrukia Ngoma na kupewa kadi nyekundu, hata hivyo ni mashabiki wachache tu waliomlaumu kwa ‘ujasiri’ wa kumrukia Ngoma wakat tayari ana kadi ya njano. Wengi walielekeza lawama kwa mwamuzi Jonesia Rukyaa.
Juuko naye ana sifa ya kucheza rafu ambazo huhitaji mwamuzi makini kuziona. Bila ya kujali athari zake, mara nyingi utawaona mashabiki wa Simba wakigongeana tano huku nyuso zao zikibebwa na tabasamu kubwa kila Juuko anapocheza kibabe bila kuonywa na mwamuzi.
Sifa hii ya ubabe inalikoroga zaidi benchi la ufundi la Simba kwani ni hatari kuwachezesha wote kwa pamoja. Hofu ya kucheza pungufu ni kubwa. Wanahitaji kucheza sambamba na Method Mwanjale.

No comments:
Write comments