Saturday, 25 March 2017

Waziri awa mbogo miradi ya maji


WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI, MHANDISI GERSON LWENGE.

WAZIRI wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Gerson Lwenge, ameonyesha kukerwa na kasi ndogo ya utekelezaji wa miradi ya maji mkoani Lindi, licha ya serikali kutoa fedha za kutosha.

Kutokana na kasi hiyo, amewataka viongozi wa mkoa kuhakikisha wanamalizia Sh. bilioni tatu kati ya Sh. bilioni tisa zilizotolewa kwa ajili ya miradi ya maji ili kupunguza tatizo la maji safi na salama linalowakabili wananchi wa mkoa huo.

Lwenge alisema hayo juzi alipokuwa akizungumza na wananchi wa kata ya Mingumbi wilayani Kilwa, wakati wa uzinduzi wa mradi wa maji Mingumbi- Miteja uliogharimu zaidi ya Sh. bilioni 4.7, ambao umejengwa na kampuni ya Patty Interplan Limited.

Alisema katika mwaka wa fedha 2016/2017, serikali ilitoa Sh. bilioni tisa kwa ajili ya kujenga miradi ya maji katika mkoa huo lakini katika hali ya kushangaza, hadi sasa zilizotumika ni Sh. bilioni sita tu huku Sh. bilioni tatu zikiwa hazijatumika wakati kero ya maji bado ipo.

Kwa mujibu wa Lwenge, Lindi ni miongoni mwa mikoa ambayo kiwango cha upatikanaji wa maji kiko chini ya wastani wa taifa ambayo ni asilimia 85 na kwamba serikali imejipanga kuongeza fedha za miradi ya maji katika mwaka ujao wa fedha.

“Umoja wa Mataifa unataka ifikapo 2030 Watanzania wote wawe wanapata maji safi na salama, viongozi tujitahidi fedha zinapotolewa na serikali zitumike ili kupunguza au kumaliza kabisa tatizo la maji,”alisema.

Aidha, Lwenge aliwagiza viongozi wa wilaya ya Kilwa kuweka bei ya kuuza maji ambayo wananchi waliowengi watamudu kununua na kwamba mradi huo utunze vizuri ili usiharibike kwa muda mfupi.

Alisema wananchi wahakikishe wanatunza vyanzo vya maji kwa kutolima na kufuga mifugo na serikali itachukua hatua za haraka kwa mtu atakayebainika akiharibu vyanzo hivyo.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa, Zablon Bugingo, alisema mradi huo ambao amekamilika kwa zaidi ya asilimia 90, utatoa huduma ya maji safi na salama katika vijiji sita ambavyo ni Kililima, Naipuli, Tingi, Mtandago, Miteja na Migumbi.

“Lengo kuu la mradi huu ni kuboresha huduma ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa umbali usiozidi mita 400 na kuongeza asilimia ya watu wanaopata maji kutoka asilimia 48.3 kwa sasa na kufikia asilimia 65.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Patty Interplan Limited, Patrick Mbedule,  alisema atahakikisha miradi hiyo inakamilika kwa muda uliopangwa kama ilivyo kwenye mkataba.

No comments:
Write comments