Mvua zinazoendelea kunyesha
zimesababisha athari kubwa katika maeneo ya Chalinze, ambapo mpaka sasa
hakuna mawasiliano ya barabara kutoka Kata ya Vigwaza na Mwavi Jimbo la
Chalinze.
Aidha, hali hiyo imesababisha wakazi
wa maeneo hayo kuvushwa kwa msaada wa kubebwa mgongoni na shingoni kwa
gharama ya sh.3,000 na 2,000 na pikipiki kupitishwa kwa sh.5,000 huku
magari yakishindwa kupita kabisa.
Mmmoja wa wakazi wa maeneo
yaliyoathirika, Zinabu Zuberi aliyekuwa akivushwa kuelekea upande wa
pili amesema kuwa wanaiomba Serikali kutoa huduma ya dharula ya
mawasiliano kwani kwa sasa wanapata shida hasa kipindi hiki cha Mvua.
“Barabara ni mbovu kama mnavyojionea,
haipitiki watu tunapata shida kufuata mahitaji ya nyumbani ,tatizo hapa
ni barabara imejengwa bila kuwekewa makaravati ndio maana imesombwa
yote na maji,”amesema Zainabu.
Hata hivyo, Mbunge wa Jimbo hilo,
Ridhiwani Kikwete amesema kuwa hali iliyopo kwa sasa hairidhishi na
inampa wakati mgumu na wakazi wa maeneo hayo, hivyo ameahidi kuisimamia
kero hiyo kwa kuifikisha Bungeni na Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze
ili lifanyiwe kazi.
No comments:
Write comments