Baada ya tukio la utekaji wa wasanii wa muziki wa bongo
fleva hapa nchini kutokea siku chache zilizopita na baadaye kupatikana,
limesababisha kutanda kwa hofu kubwa miongoni mwa wasanii wa muziki huo
hali ambayo imepelekea Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo,
Dkt. Harrison Mwakyembe kujitokeza hadharani kulaani kitendo hicho na
kuahidi kuwashughulikia wale wote waliohusika.
Ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar
es Salaam, Waziri huyo amesema kuwa amesikitishwa sana na kitendo hicho
hivyo ameahidi kulishughulikia jambo hilo kwa haraka zaidi ili wahusika
wakamatwe na wachukuliwe hatua kali za kisheria.
“Hiki kilichotokea siyo hali ya kawaida kwa watanzania, hatuwezi
kukubali kitu kama hiki kiendelee kutokea,nitalifuatilia kwa ukaribu
sana, nitajitahidi nipate majibu kabla ya bajeti yangu Bungeni”. Dkt.
Mwakyembe
Hata hivyo Dkt. Mwakyembe amewataka wasanii wote nchini kutoa
taarifa Ofisini kwake pindi tu wanapoona kuna tatizo au mtu yeyote
anawasumbua kuhusu suala zima la sanaa kwani yeye ndiye Waziri mwenye
dhamana na si mwingine.
Kwa upande mwingine, Mwakyembe ameongeza kuwa ameagiza vyombo vya
dola kufanya uchunguzi wa haraka zaidi katika tukio hilo baya la utekaji
kwani siyo la kawaida kutokea hapa nchini.
Pia Waziri huyo mwenye dhamana na wasanii ametoa ujumbe kwa vyombo
vyote vilivyopo chini ya Wizara yake kutofanya mahojiano yoyote
yanayowahusu wasanii hao bila ya kuwepo taarifa kamili kutoka kwake.
No comments:
Write comments