Wanawake wa Chadema wamemtwishwa Regina Lowassa mzigo wa kuongoza mapambano ya ushindi katika Uchaguzi Mkuu wa 2020.
Akizungumza
na wajumbe wa Baraza Kuu la Wanawake wa Chadema (Bawacha) mjini Dodoma
jana, Regina ambaye ni mke wa waziri mkuu wa zamani Edward Lowassa,
alisema maandalizi ya uchaguzi huo yanapaswa kuanza sasa.
Katika
Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, Lowassa aligombea urais kupitia Chadema
kwa kushirikiana na vyama vilivyounda umoja wa katiba ya Wananchi
(Ukawa) na hivyo kuweka ushindani mkubwa dhidi ya chama tawala, ingawa
hakushinda.
Jana,
Regina alisema ushindi wa chama hicho uko mikononi mwa wanawake wa
Tanzania. “Kwanza niwashukuru sana kwa mapambamo mliyoyafanya mwaka
2015. Nataka mfahamu kuwa bado Chadema inapendwa na ina nguvu kubwa
kuliko wakati mwingine. Msikatishwe tamaa bali tusonge mbele,” alisema
Regina.
Mama
huyo aliwataka wajumbe kujiamini zaidi na kupeleka ujumbe kwa wenzao
ambao wamedhamiria kufanya mageuzi makubwa, lakini akawataka wasilale.
Mwenyekiti
wa Bawacha, Halima Mdee aliwataka wanawake kujitoa zaidi katika
kukisaidia chama hicho, hasa katika maandalizi ya uchaguzi ujao.
Mdee aliwashauri wanawake wenye nafasi, kama wabunge, kutumia nafasi zao kukisaidia chama.
Alisema
wakati walionao kwa sasa si wa kujivunia nafasi walizonazo, bali
wanapaswa kuongeza nguvu zaidi na kugombea nafasi za uongozi wa juu wa
Chadema ili waendeleze mapambano ya ukombozi.
“Katika
kipindi hiki ambacho tunaona demokrasia inaminywa kwa vyama vyote vya
siasa, ni vema wanawake ambao ni jeshi kubwa tukawa mstari wa mbele
katika mapambano si kurudi nyuma. Lazima kuwa na nidhamu ndani na nje ya
chama ili tufanikiwe katika vita hii,” alisema Mdee.
Katika
kuonyesha msisitizo huo, alimuagiza katibu mkuu wa Bawacha, Grace
Tendega kuwaandikia barua wabunge ambao hawakuhudhuria kikao cha jana
ili wajieleze kabla ya kuchukuliwa hatua.
Alisema
ni jambo la aibu na fedheha kwa viongozi kutoka mbali wakasafiri hadi
Dodoma kwa ajili ya kikao, lakini wabunge ambao wako mjini hapa
wakashindwa kuhudhuria.
Mbunge
wa Viti Maalumu, Devotha Minja alisema chachu ya ushindi na mapambano
ndani ya chama hicho kwa sasa ni kubwa kwa kuwa wameamua kufanya kazi
usiku na mchana kwa ajili ya kuisaidia Chadema.
No comments:
Write comments