Wakati hofu ikiwa imetenda baada ya jumla ya miezi minane kupita tangu
alipopotea kwenye mazingira ya kutatanisha, matumaini mapya yameanza
kuibuka baada ya simu yake kuonekana imetumika kwenye mitandao ya
kijamii.
Ben Saanane ambaye alikuwa msaidizi wa Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman
Mbowe alitoweka mwaka jana na kumekuwapo na hisia nyingi kuwa huenda
alishafariki dunia kutokana na kuwa, hakuna yeyote anayefahamu alipo
kijana huyo aliyekuwa akichipukia katika siasa nchini Tanzania.
Kwa mujibu wa gazeti la TanzaniaDaima, simu ya Ben jana alitumika majira
ya saa tatu asubuhi ambapo ilionekana namba yake ikijitoa kwenye
makundi ya WhatsApp. Imeelezwa kuwa namba yake ilijitoa kwenye makundi
mengi huku ikiwaacha na mshangao mkubwa wajumbe (members) wa makundi
hayo.
Hofu ya kuwa kijana huyo hayupo hai ilichangiwa na jibu alilolitoa
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa bungeni ambapo alisema, “familia ya mtajwa
(Ben Saanane) aliyetangulia mbele za haki au vinginevyo, uchunguzi wa
suala lake utakapokamilika, taarifa rasmi itatolewa.”
Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo alipokuwa akijibu swali la Kiongozi wa
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe Aprili 20 mwaka huu
aliyetaka kujua kwanini serikali imekuwa kimya sana kwenye suala la
kupotea kwa msaidizi wake.
Namba ya Ben Saanane iliyotoka kwenye makundi ya whatsapp ni 0768078523
ambayo imesajiliwa kwa jina lake na amekuwa akiitumia kabla ya kutoweka.
Makundi ambayo namba hiyo inadaiwa kujitoa ni pamoja na Jukwaa la Siasa,
Chadema Tanzania, Friends of Bavicha, Tanzania nchi yetu sote na Bantu
Politics Tz Kwanza.
Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano, Uenezi na Mambo ya Nje wa CHADEMA,
John Mrema alisema kuwa tukio hilo limewashtua sana kuona mtu ambaye
ametoweka simu yake ikitumika kujitoa kwenye makundi ya whatsapp. Aidha,
alihoji Polisi wanachukua hatua gani kujua alipo au simu yake ilipo.
Kwa upande wa familia yake, Erasto Saanane ambaye ni mdogo wake Ben
alisema kuwa hawajui kama ni yeye au ni nani anatumia simu hiyo kwani
hata kwenye kundi la familia amejitoa.
Ndugu huyo alisema hata rafiki zake Ben walisema kwenye makundi mengine
amejiondoa pia, na kuwa Jumatano iliyopita ukurasa wake wa Facebook
ulitumika ukimuonyesha yupo Tengeru, Arusha.
Aidha baada ya kuona kaka yake amejitoa kwenye makundi hayo, alitoa
taarifa katika kituo cha polisi Tabata, na kuwa uchunguzi wa suala hilo
umeanza.
No comments:
Write comments