Kiungo wa Yanga, Haruna Niyonzima, amesikia taarifa za yeye kusaini Simba na kusema: “Simba, thubutu mnajidanganya nyie, mimi bado mchezaji wa Yanga!”
Kauli
hiyo ya Niyonzima imekuja siku moja baada ya taarifa kuzagaa kuwa,
kiungo huyo mwenye mbwembwe nyingi ndani ya uwanja, amesaini mkataba wa
miaka miwili Simba.
Niyonzima
sasa ni mchezaji huru anayeruhusiwa kufanya mazungumzo na klabu
nyingine yoyote itakayomhitaji kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Bara
kwani mkataba wake unaisha mwezi ujao.
Akizungumza
kutoka Rwanda, Niyonzima ambaye yupo katika kambi ya timu ya Taifa ya
Rwanda ‘Amavubi’, alisema hajasaini wala kufanya mazungumzo yoyote na
Simba.
Niyonzima alisema: “Ni ngumu kuchukua maamuzi hayo mimi binafsi bila ya kuishirikisha Yanga kwani kanuni zinanibana.”
Kiungo
huyo alisema, kama kuna klabu inamhitaji hivi sasa, ni vizuri ikafuata
kanuni za usajili kwa kuifuata Yanga ambao ndiyo waajiri wake kwa ajili
ya mazungumo kabla ya kumfuata yeye.
“Nikuhakikishie
tu wallah! Sijazungumza na kiongozi yeyote wa Simba kwa ajili ya
kusaini na hizo zinazoendelea ni tetesi tu pekee ambazo hazina ukweli
wowote.
“Timu
niliyofanya nayo mazungumzo ni Yanga na tumefikia makubaliano mazuri ya
mimi kuongeza mkataba mwingine wa kuendelea kubaki Jangwani.
“Kwanza
ninashindwa kuelewa ni nani anayesambaza hizo taarifa, kwa sababu ni
ngumu mimi kusaini mkataba Simba nikiwa bado nina mkataba wa mwezi mmoja
Yanga.
“Niseme
tu kuwa klabu inayonihitaji ni lazima ifuate kanuni za usajili kwa
kuwafuata viongozi wangu wa Yanga kwanza kuzungumza nao, halafu ndiyo
waje kwangu kwa baraka za uongozi.
“Niwatoe
hofu viongozi na mashabiki wangu wa Yanga kuwa, mimi bado ni mchezaji
wao na kwa sasa nipo nyumbani Rwanda nikiwa kwenye majukumu ya timu
yangu ya taifa,” alisema Niyonzima.
Juzi
Alhamisi, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans
Poppe, akizungumza katika Kipindi cha Spoti Hausi cha Global TV Online,
alisema anafurahishwa na uchezaji wa Niyonzima, Donald Ngoma na Obrey
Chirwa wote wa Yanga.
“Ngoma,
Chirwa na Niyonzima wote wana nafasi ya kucheza Simba, mimi binafsi
ningependa hawa wacheze Simba kama inawezekana,” alisema Hans Poppe.
Niyonzima ni mshindi wa Tuzo ya Mchezaji Bora wa Kigeni kwa msimu uliopita wa Ligi Kuu Bara wa 2016/17.
No comments:
Write comments