Waziri Mkuu wa zamani na mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa
amesema licha ya changamoto nyingi anazopata akiwa ndani ya upinzani,
atagombea tena urais katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2020 na anaamini
atashinda.
Lowassa aliyejitokeza kugombea urais kupitia CCM mwaka 2015 na jina lake
kukatwa kisha kuhamia Chadema alikogombea nafasi hiyo akiwakilisha
vyama vilivyoungana chini ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na
kushindwa na Rais John Magufuli, bado anatajwa kuwa mgombea mwenye nguvu
katika kambi ya upinzani.
Kwa mujibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Rais Magufuli alishinda
kwa kupata kura 8,882,935 sawa na asilimia 58.46, huku Lowassa wa
Chadema akijipatia kura 6,072,848 sawa na asilimia 39.97 ya kura zote.
Akizungumza jana katika mahojiano maalumu na waandishi wa Nation Media
Group (NMG) jijini Nairobi, Lowassa alisema, “Kwa mapenzi ya Mungu
nitajaribu tena mwaka 2020 na nitapita kwa mikono safi.”
Kama ambavyo amekuwa akisema tangu aliposhindwa katika uchaguzi huo wa
2015, pia jana Lowassa alisema licha ya kuendeshwa katika mfumo
usioaminika, hakutaka kuwashawishi wafuasi wake wamwage damu kwa kudai
ushindi.
“Wafuasi wangu walitaka tuingie mitaani kudai ushindi, lakini kulikuwa
na bunduki nyingi mikononi mwa wanajeshi. Niliogopeshwa na umwagikaji wa
damu. Sikutaka kuingia Ikulu kupitia damu za watu kwa sababu sistahili
hivyo,” alisema.
Hata hivyo, alisema licha ya uchaguzi huo kutoaminika, bado anamheshimu
Dk Magufuli kama Rais, japo mbunge huyo wa zamani wa Monduli alikataa
kukubaliana na utendaji wa mkuu huyo wa nchi kwa kipindi alichokaa
madarakani.
“Hata kama Dk Magufuli alichaguliwa katika mfumo usioaminika wa
uchaguzi, bado tunamheshimu kama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania,” alisema Lowassa. Alisema, “Utendaji wa Rais Magufuli
utaamuliwa na watu utakapofika mwisho wa muhula huu mwaka 2020. Bora
niwe makini katika hili nisije nikanukuliwa vibaya nikaingia kwenye
matatizo nitakaporudi nyumbani.”
Lowassa ambaye hivi karibuni amekuwa akiripoti Makao Makuu ya Jeshi la
Polisi jijini Dar es Salaam kutokana na kauli yake kuhusu viongozi wa
Jumuiya ya Uamsho waliokamatwa mwaka 2012 huko Zanzibar, alilaani
ukiukwaji wa demokrasia akisema Chadema itakwenda mahakamani kudai haki
ya kufanya siasa.
“Kukataza huko siasa ni kinyume cha demokrasia na haki, hata hivyo
tunajitahidi kujiimarisha. Tumeshalalamika serikalini kuondoa katazo
hilo lakini bado inajivuta miguu. Tunaweza kulazimika kwenda kutafuta
msaada wa Mahakama,” alisema.
Kuhusu kamatakamata ya viongozi wa upinzani, Lowassa alisema licha ya
kupata zaidi ya kura milioni sita, ameshindwa hata kuwashukuru wananchi
waliompigia kura.
“Nilipata kura milioni sita na siwezi kufanya mikutano hata ya
kuwashukuru watu kwa kunipigia kura. Hiyo si tu kinyume cha demokrasia,
bali si haki,” alisema Lowassa.
Wakati Jeshi la Polisi likikataza vyama vya upinzani kufanya mikutano ya
hadhara mwaka 2016, Rais Magufuli alisema wanasiasa waliochaguliwa
wanaweza kufanya mikutano kwenye majimbo yao.
Hata hivyo, bado baadhi ya mikutano ya ndani ya vyama hivyo imeendelea kuzuiwa na viongozi wa upinzani wakikamatwa.
Licha ya kukiri kuwa ndani ya upinzani kuna changamoto nyingi, Lowassa
alisema kuna wakati anapata faraja kuwa upande huo wa siasa.
“Ni uzoefu mzuri unaoendana na nyakati nzuri na ninafurahia uzoefu huo
kwa sababu mimi bado ni maarufu na nina wafuasi wengi. Kukataza shughuli
za siasa ni hatua ya kuninyamazisha,” alisema.
Lowassa alisisitiza msimamo wa Chadema wa kumuunga mkono Rais wa Kenya,
Uhuru Kenyatta katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Agosti 8
akisema kiongozi huyo ni chaguo sahihi kwa demokrasia za Kenya.
“Tumekuwa na vikao halali kama chama na vya wazi na kukubaliana kumuunga
mkono Uhuru Kenyatta achaguliwe tena. Ni mtu mzuri anayeunga mkono
Jumuiya ya Afrika Mashariki na anaheshimu viongozi wa upinzani,”
alisema.
Hata hivyo, Lowassa aliyekwenda Kenya kuhudhuria mazishi ya aliyekuwa
Waziri wa Usalama, Jenerali Joseph Nkaisery alifafanua kuwa uamuzi wa
kiongozi sahihi wa kuiongoza Kenya utafanywa na Wakenya wenyewe kwenye
uchaguzi wa Agosti.
Alipoulizwa ni kwa nini Chadema imebadilisha mgombea wanayemuunga mkono
katika uchaguzi wa Kenya, kutoka kwa Raila Odinga wa Nasa, Lowassa
alisema amekuwa akimuunga mkono Kenyatta kwa muda mrefu.
Kabla Lowassa hajajiunga na Chadema, Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman
Mbowe alishatangaza kumuunga mkono Odinga wakati huo akiwa Waziri Mkuu
wa Kenya.
No comments:
Write comments