WAGOMBEA wawili wa nafasi ya Urais
na mmoja wa nafasi ya Makamu wa Rais katika Chama cha Wanasheria
Tanganyika (TLS), Tundu Lissu na Lawrence Masha, wamewasilisha maombi ya
kujumuishwa kama wadaiwa katika kesi ya kupinga kufanyika kwa uchaguzi
wa TLS.
Mwingine aliyepeleka maombi hayo katika
kesi iliyofunguliwa na Wakili Godfrey Wasonga wa Dodoma, ni Godwin
Ngwilimi anayewania nafasi ya Makamu wa Rais wa TLS katika uchaguzi
unaotarajiwa kufanyika Jumamosi wiki hii jijini Arusha.
Shauri hilo liko mbele ya Jaji Awadhi
Mohammed wa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma. Katika chemba ya Mahakama Kuu
jana, Ngwilimi alisema ni miongoni mwa waleta maombi ya kuunganishwa
katika shauri hilo.
Kwa upande wake, Lissu ambaye pia ni
Mbunge wa Singida Mashariki kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), alisema “nina maombi ya kuunganishwa kwenye shauri hili,
tumeomba mimi na Lawrence Masha, kwani tuna mashaka makubwa na kanuni
zilizotumika.” Hata hivyo, Jaji Mohammed alisema hajapokea rasmi maombi
ya waleta maombi hayo.
Alitaka wadaiwa wengine katika shauri hilo, Mwanasheria Mkuu waSerikali (AG) na TLS waandikiwe mwito wa kuitwa mahakamani.
“Application sijaiona, siwezi kuzungumza
chochote, inaonekana TLS wahusika wake wako Dar es Salaam, ni muhimu
wakapewa mwito wa kuitwa mahakamani,” alisema Jaji Mohammed na kuongeza
kuwa shauri hilo litaendelea kesho na kutaka AG na TLS wawepo mahakamani
na maombi ya kutaka kuunganishwa kwenye shauri hilo yatasikilizwa na
kutolewa maamuzi.
Akizungumza nje ya mahakama, Lissu alisema
wamefanya uamuzi huo kama njia ya kuuongezea nguvu upande wa wadaiwa
kutokana na kesi iliyofunguliwa na Wasonga.
Alisema uchaguzi huo umekuwa ukifuatiliwa
kwa karibu na watu wengi huku akibainisha kuwa kuna kile alichokiita
njama dhidi ya kuuharibu uchaguzi.
“Baada ya kupata fununu kesi imefunguliwa
tukafuta nakala, lakini madai yaliyopo hayana mashiko kwani zaidi ya
miaka 65 TLS ipo, lakini jambo la kupinga uchaguzi ndio linajitokeza
sasa,” alisema Lissu na kudai `figisu figisu’ za uchaguzi huo ni baada
ya kuona wagombea wa safari hii wataleta mabadiliko kutokana na TLS kuwa
mfu miaka mingi.
Alisema mambo yenye uhusiano na kikatiba
na kisheria yamekuwa yakipita bila TLS kuwa na mchango wowote. Alisema
wenye hofu wamejitokeza na kudai wanasiasa wamevamia uchaguzi huo.
“Sheria zilizoanzisha TLS hazina katazo la
aina hiyo, sifa kubwa ni wakili anayelipa ada na kupata hati ya kufanya
kazi mahakamani,” alidai.
Kwa upande wake, Wakili Wasonga alisema kuna kanuni ambazo zinakinzana na sheria za TLS .
“Baada ya kuzisoma kanuni niliona
zinakinzana na sheria za TLS, zimekuwa za kibaguzi hazitoi fursa na
nafasi sawa katika kugombea, hazitoi mwanya wa kukata rufaa,” alieleza
Wasonga na kubainisha kuwa baada ya Lissu na Masha kupeleka mahakamani
maombi ya kuunganishwa kwenye shauri hilo, mahakama itaona wanastahili
au la
No comments:
Write comments