Wakati mabadiliko ya katiba
yatawaengua vigogo 11 katika uongozi wa CCM walio na kofia zaidi ya
moja, hatima ya idadi kama hiyo ya wanachama wanaodaiwa kukisaliti chama
hicho wakati wa Uchaguzi Mkuu uliopita, itajulikana kesho.
CCM inatarajia kupitisha mabadiliko
makubwa ya katiba, ambayo yatapunguza idadi ya wajumbe katika vikao vya
juu na pia kupunguza kofia za uongozi mwanachama mwenye cheo ndani ya
chama, ubunge au serikalini.
Mabadiliko hayo yalipendekezwa na Halmashauri Kuu ya CCM, iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam Desemba 13 mwaka jana.
Mabadiliko hayo yalitangazwa kwenye vyombo
vya habari na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM aliyemaliza muda wake,
Nape Nnauye kwamba muundo wa chama umebadilika na mwanachama anatakiwa
kuwa na nafasi moja tu ya uongozi wa kazi za muda wote kama
ilivyoainishwa kwenye Kanuni za Uchaguzi wa CCM, Toleo la 2012, Kifungu
cha 22 na 23.
Nape alizitaja nafasi hizo kuwa ni
mwenyekiti wa tawi, kijiji au mtaa, kata/wadi, jimbo, wilaya na mkoa.
Wengine ni makatibu wa halmashauri kuu wa ngazi zote, mbunge, mwakilishi
na diwani.
Mabadiliko hayo pia yamepunguza ukubwa wa
Kamati Kuu kutoka wajumbe 34 hadi 24, hali inayofanya wanaoingia kwa
kupigiwa kura kupungua hadi wanne kutoka kumi.
Pia nafasi za ujumbe wa Halmashauri Kuu
zimepungua kutoka 388 hadi 158, huku wengi wakiingia kwa nafasi zao na
wajumbe kutoka wilayani kuondolewa.
Kutokana na mabadiliko hayo, baadhi ya
viongozi wenye kofia zaidi ya moja wameshaanza kutangaza kutotetea
nafasi zao katika uchaguzi ujao wa viongozi wa CCM na jumuiya zake.
Wa kwanza alikuwa Sophia Simba ambaye ni
mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT) Sophia Simba. Simba pia mbunge na
mjumbe wa Kamati Kuu.
Mwingine ni Abdallah Bulembo aliyetangaza
kuwa hatagombea uenyekiti wa Umoja wa Wazazi wa CCM. Bulembo ameteuliwa
na Rais Rais John Magufuli kuwa mbunge, jambo linalomfanya awe na kofia
mbili.
Mbali na hao waliotangaza hadharani, wapo
vigogo wengine ambao wana nafasi zaidi ya moja za uongozi, akiwamo
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi ambaye
mbali na uwaziri ni mbunge, mjumbe wa NEC na mjumbe wa Kamati Kuu.
Pia Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo
ya Makazi, William Lukuvi ni mbunge na mjumbe wa Kamati Kuu, kama ilivyo
kwa Profesa Makame Mbarawa (Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano)
ambaye ni mjumbe wa Kamati Kuu wakati Shamsi Vuai Nahodha ni mbunge na
mjumbe wa Kamati Kuu.
Mabadiliko hayo pia, yatawakumba wenyeviti
wa CCM wa mikoa ambao kwa nafasi zao ni wajumbe wa NEC. Mmojawapo ni
Kimbisa, ambaye ni mwenyekiti wa Mkoa wa Dodoma na mjumbe wa Kamati Kuu.
Wenyeviti wa mikoa ambao pia ni wabunge ni
Joseph Msukuma (Geita), Martha Mlata (Singida) na Deo Simba (Njombe).
Mwenyekiti wa CCM wa Mbeya, Godfrey Zambi pia ni mjumbe wa NEC na mkuu
wa Mkoa wa Lindi.
Mwingine anaonekana kuguswa na mabadiliko
hayo ni Salma Kikwete ambaye ni mjumbe wa NEC anayewakilisha Wilaya ya
Lindi Mjini na ambaye hivi karibuni aliteuliwa na Rais kuwa mbunge.
Maoni ya CCM, Mbunge Njombe
Alipoulizwa kuhusu mabadiliko hayo, naibu
katibu mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai alisema suala la kofia mbili
litajadiliwa na kutolewa uamuzi na Halmashauri Kuu.
“Tusiwahishe ajenda hiyo. Hatuzuii mtu
kujiuzulu kwa utashi wake, lakini jambo hilo litajadiliwa na Kamati Kuu
na mwishowe kwenye Halmashauri Kuu chama kitaweka wazi nini kitafanyika
kwa sababu huko ndipo yatangazwa mabadiliko ya kanuni na ratiba ya
uchaguzi ndani ya chama utakavyokuwa kuanzia ngazi ya matawi,” alisema
Vuai.
Mbunge wa Njombe Kaskazini, Deo Sanga ni
miongoni mwa wanachama wenye kofia mbili, akiwa pia mwenyekiti wa CCM wa
Mkoa wa Njombe. Alipoulizwa atavua kofia gani kati ya ubunge na
uenyekiti, alisema anasubiri mwongozo wa Halmashauri Kuu.
“ Mimi ni mjumbe natarajia kwenda huko
huko. Mwongozo ukitolewa ndipo nitajua cha kufanya, lakini kwa sasa
siwezi kukueleza kwa uhakika,” alisema Sanga.
Wengine waliotafutwa kuzungumzia suala hilo hawakupatikana, isipokuwa Msukuma ambaye alisema yuko kikaoni.
Hatua kali za kinidhamu
Lakini hoja inayotarajiwa kutingisha ni ya
kujadili mchakato wa uteuzi wa wagombea wa CCM na mambo yaliyojitokeza
katika kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Miongoni mwa wanachama watakaokuwa katika
wakati mgumu ni wajumbe watatu wa Kamati Kuu ambao walipinga hadharani
maamuzi ya chombo hicho ya kupitisha majina matano ya wagombea urais kwa
maelezo kuwa katiba ya CCM ilikiukwa.
Wajumbe hao ni Sophia Simba, Adam Kimbisa na Emmanuel Nchimbi.
Waliopitishwa walikuwa Bernard Membe,
January Makamba, Dk Asha-Rose Migiro, Balozi Amina Salum Ali na John
Magufuli (ambaye alishinda na sasa ndiye Rais).
Chanzo cha habari kililiambia Mwananchi
kuwa baadhi ya wanachama hao wameshahojiwa na Kamati ya Maadili na
kwamba kinachosubiriwa sasa ni uamuzi.
“Kamati ya maadili imeshamuhoji Sophia
Simba na wanachama wengine na NEC inakaa na kupokea mapendekezo ya
Kamati ya Maadili, hapo ndiyo hatma yao itajulikana. Lakini nakwambia
ndugu yangu hawa watu sasa hawawezi kutoka,” alisisitiza.
Mwananchi ilipomtafuta Simba kuhusu suala hilo alisema hayo ni maneno ya mtaani na kwamba chama kina taratibu zake.
“Chama kina taratibu zake hakiwezi
kuyumbishwa na maneno ya mitaani. CCM ina taratibu zake na maamuzi
yanapitia vikao halali vya chama,” alisema Simba.
“Kwanini unataka tuvuke mto ilihali hatujafika.”
Alipoulizwa kuhusu taarifa kuwa alihojiwa pamoja na watuhumiwa wengine, alisema hizo ni taratibu za kawaida katika chama chao.
“Ninachofahamu kuhojiwa ni taraibu za kawaida sina kesi yoyote,” alisema.
Juhudi za Mwananchi hazikufanikisha
kumpata Kimbisa, hali kadhalika Nchimbi ambaye kwa sasa ameteuliwa kuwa
balozi nchini Brazil kutokana na simu zao kutopatikana.
Wengine watakaokuwa katika wakati mgumu ni
wanachama wanaodaiwa kukisaliti chama wakati wa kampeni za uchaguzi na
ambao walijadiliwa kuanzia ngazi ya wilaya na baadaye mapendekezo
kuwasilishwa vikao vya juu na baadaye Kikwete kumkabidhi Rais Magufuli
ripoti hiyo.
Mara kadhaa viongozi wa chama hicho
walikaririwa wakitaka wasaliti wa chama kuchukuliwa hatua, akiwamo
Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan ambaye aliwataka viongozi wa CCM wa
Mkoa wa Kaskazini A kisiwani Unguja kuwachukulia hatua zinazostahili
wanachama wanaokisaliti na kukihujumu chama.
Pia, mara kadhaa wakati wa kampeni, Rais
Magufuli alikuwa akituhumu wanachama kuwa walikuwa wakionyesha kuwa CCM
mchana na usiku wakipigia kampeni wagombea wa vyama vilivyounda Umoja wa
Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Katika uchaguzi huo, vyama vya upinzani
viliendelea kuipokonya CCM viti huku mgombea urais aliyeungwa mkono na
Ukawa, Edward Lowassa akipata takriban asilimia 40 ya kura zote, ikiwa
ni mara ya kwanza tangu uchaguzi wa vyama vingi urudishwe mwaka 1995.
Wanachama wanaodaiwa kukisaliti chama
hicho ni pamoja na mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Iringa, Jesca
Msambatavangu, ambaye amekuwa akilalamikiwa kutokana na CCM kufanya
vibaya katika uchaguzi wa jimbo la Iringa Mjini lililochukuliwa tena na
Mchungaji Peter Msigwa wa Chadema.
Bulembo ajiuzulu
Katika hatua nyingine, jana katika kikao
cha Baraza Kuu Maalum la Jumuiya ya Wazazi, Bulembo alitangaza kutotetea
nafasi yake ya unyekiti.
“Kila mmoja ni shahidi, wakati naingia,
jumuiya hii ilikuwa inakwenda kufa, jambo lililosababisha aliyekuwa
mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete kutaka kuifuta. Lakini
nikamuhakikishia ataona mapinduzi akiniachia,” alisema Bulembo.
“Sasa natoka kifua mbele, yale yote
niliyoyaahidi nimetimiza kwa asilimia 75. Tangu nimeingia hatujawahi
kuomba hata shilingi moja kwa ajili ya uendeshaji,” alisema.
Hata hivyo, Bulembo alisema ataendelea na vikao vyote mpaka Oktoba atakapomkabidhi rasmi mwenyekiti mpya.
Alisema kwa sasa asiulizwe kwa nini
amechukua uamuzi huo na kwamba hoja siyo kuteuliwa kwake kuwa mbunge
bali ni utaratibu aliojiwekea katika maisha yake.
Credit – Mwananch
No comments:
Write comments