VINASABA vya faru John vinatarajiwa
kupelekwa nchini Afrika Kusini kwa vipimo vya vinasaba (DNA ) muda
wowote kuanzia wiki hii baada kupatikana kwa mfadhili wa kulipia gharama
za vipimo hivyo,
Faru John alizua gumzo nchini mwishoni mwa
mwaka jana baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kufanya ziara katika
Hifadhi ya Bonde la Ngorongoro (NCAA) na kuwatuhumu maofisa wa shirika
hilo na wale wa Idara ya Wanyamapori kwa ‘kumuuza’ faru John kwa kampuni
ya Grumeti kwa takriban shilingi milioni 200.
Kutokana na tuhuma hizo maofisa zaidi ya
watano kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Idara ya Wanyapori na
Tawiri walitiwa mbaroni kwa mahojiano na vyombo vya usalama. Hata hivyo,
baada ya muda maofisa hao waliachiwa huru.
Kampuni hiyo ya Grumeti ambayo imewekeza
katika shughuli za biashara ya hoteli, utalii na uhifadhi inamiliki
hifadhi ndogo (sanctuary) ya Faru Weusi pembezoni mwa Hifadhi ya Taifa
ya Serengeti.
Aidha katika mfululizo wa matukio kuhusu
sakata la faru huyo baadaye ilibainika alifariki dunia Agosti mwaka jana
na waziri mkuu aliunda kamati maalumu kuchunguza kifo chake na pia
kupimwa DNA.
Taarifa zilizofika kutoka ndani ya Wizara
ya Maliasili na Utalii zimeeleza kuwa tayari nyaraka zote muhimu kuhusu
kupelekwa kwa vipimo hivyo nchini humo zimekamilika.
Habari zaidi zinaeleza kuwa pamoja na
kukabidhi nyaraka, maofisa wa Wizara ya Maliasili na Utalii watakabidhi
pia sampuli za vinasaba hivyo kwa ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali ili
visafirishwe kwenda Afrika Kusini.
Awali ilidaiwa kuwa kulikuwa na hali ya
utata kuhusu nani hasa atalipa gharama za vipimo hivyo vya DNA baada ya
Wizara ya Maliasili na Utalii kushindwa kupata fedha za kugharimia
vipimo hivyo.
“Taarifa ni kwamba kuna mfadhili
amepatikana (hakutaja jina) na kulipia gharama za vipimo vya DNA nchini
Afrika Kusini katika maabara ya kupima vinasaba ambayo iko kitivo cha
wanyama katika Chuo Kikuu cha Pretoria,” kilieleza chanzo chetu ndani ya
Wizara hiyo.
Chanzo hicho kiliongeza kuwa gharama za
vipimo hivyo ni katika ya dola za Marekani 300,000 hadi 500,000 ambazo
ni zinaweza kufikia kati ya shilingi za Tanzania milioni 700 hadi
bilioni moja.
“Kwa kweli gharama za kufanya vipimo vya
DNA ziko juu sana na serikali haikuwa na fedha zilizotengwa kwa kazi
hiyo, amepatikana mfadhili ambaye atalipia gharama hizo hivyo muda
wowote kuanzia sasa vipimo vitapelekwa Afrika Kusini baada ya kukamilika
kwa nyaraka zote muhimu,” alieleza mmoja wa maofisa wa wizara hiyo
aliyeomba asitajwe jina gazetini kwa kuwa si msemaji wa suala hilo.
Majibu ya vipimo hivyo ndiyo
yanayotarajiwa kutengua kitendawili cha iwapo sampuli za vinasaba
zilizochukuliwa kutoka katika mabaki ya mnyama huyo zinaoana na zile
zilizoko kwenye pembe yake na kujua iwapo faru huyo alikufa kama
watendaji wa Idara ya Wanyapori wanavyodai au la.
Juhudi za kumpata msemaji wa Wizara ya
Maliasili na Utalii Dorina Makaya hazikuweza kufanikiwa kutokana na simu
yake kutokuwa hewani kwa muda mrefu lakini Afisa Mawasiliano wa Wizara
hiyo, Hamza Temba, alisema kwa kifupi kuwa suala hilo liko chini ya
Ofisi ya Waziri Mkuu na pia Mkemia Mkuu wa Serikali.
“Sidhani kama jambo hilo liko chini ya
wizara kwa kifupi ninavyofahamu suala hilo liko chini ya ofisi ya waziri
mkuu na pia mkemia mkuu wa serikali,” alisema ofisa huyo.
Maabara ya Chuo Kikuu cha Pretoria nchini
Afrika Kusini ( Veterinary Genetics Laboratory – VGL)) kwa mujibu wa
mtandao wa researhmatters.up.ac.za ilianzishwa mwaka 2009 baada ya
kuwapo kwa wimbi kubwa la ujangili dhidi ya wanyama hao nchini humo.
Kwa mujibu wa mtandao huo wataalamu wa
chuo hicho kitivo cha utafiti na tiba ya wanyama wakiongozwa na Dk.
Cindy Harper walifikia uamuzi wa kuanzisha maabara hiyo kwa lengo la
kukusanya sampuli za vinasaba kutoka kwa wanyama hao na kuhifadhi katika
kanzidata (database) ya maabara ili zitumike kama sehemu ya ushahidi
mahakamani katika kesi za ujangili wa faru.
Ugunduzi na uamuzi wa wataalamu hao
ulitokana na kesi nyingi dhidi ya majangili kukwama na wengi kuachiwa
huru baada ya kukosekana kwa ushahidi dhidi yao.
Kwa mujibu wa mtandao huo wataalamu hao wa
chuo hicho hutumia sampuli za vinasaba na kuoanisha na alama za vidole
vya majangili kisha kuwapa waendesha mashitaka ili kujenga ushahidi
thabiti wa kuwatia hatiani washitakiwa.
Takwimu zinaonyesha kuwa dunia ina faru
wasiozidi 29,000 kati ya faru 500,000 waliokuwepo mwanzoni mwa karne ya
20 na Afrika Kusini ndiyo nchi inayoongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya
wanyama hao kwa sasa.
Kutokana na ujangili wa muda mrefu dhidi
ya faru na mahitaji ya pembe zake katika nchi za kiarabu na zile za Asia
ya Kusini ambazo wakati mwingine hutumika kama dawa za kiasili
kumesababisha dunia kubakiza karibu asilimia moja tu ya faru.
Nchini Afrika Kusini pekee kati ya mwaka
2010-2015 zaidi ya faru 500 waliuawa na majangili na mwaka 2013 ulivunja
rekodi kwa faru 1,008 kuuawa na majangili.
Kwa upande wake Waziri wa Maliasili na
Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, alishindwa kulitolea ufafanuzi suala
hilo kwa maelezo kuwa alikuwa katika kikao cha wajumbe wa Kamati ya
Bunge ya Ardhi, Mazingira na Maliasili
No comments:
Write comments