Monday, 6 March 2017

Wabunge Upinzani Wamtetea Mwenzao Aliyekosolewa na Rais Magufuli

Wabunge wa upinzani na wasomi wamekuwa na mawazo kinzani kuhusu maswali na kauli alizotoa Rais John Magufuli juzi mbele ya wananchi wa Somanga dhidi ya Mbunge wa Jimbo la Kilwa Kaskazini, Vedasto Ngombale (CUF).
Ilikuwa ni siku moja baada ya Ngombale kukataa ushauri wa Rais Magufuli wa kumtaka achangie angalau Sh15 milioni kutoka mfuko wa jimbo kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya.
Tukio hilo lilitokea eneo la Somanga Wilaya ya Kilwa wakati Rais Magufuli aliposimama kwa muda kuongea na wananchi baada ya kuanza ziara yake katika mikoa ya Pwani, Lindi na Mtwara.
Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Richard Mbunda alisema vita ya kupambana na upinzani kwa sasa imekuwa wazi na mwenyekiti wa CCM (John Magufuli) amekuwa akitumia kila nafasi anayoipata kuwamaliza wapinzani.
“Ni mentality (mtazamo) ya mwanasiasa yeyote, Rais Magufuli angetamani majimbo yote yawe ya chama chake, kwa hivyo akipata mwanya kama huo lazima awamalize,” alisema.
Hata hivyo, Mbunda alisema maendeleo ya wananchi hutekelezwa na halmashauri na mbunge kazi yake ni kuchochea wananchi kuanzisha na kushiriki miradi, ikiwamo kushawishi Serikali kupitia Bunge ili kushughulikia changamoto zilizopo.
“Lakini, fedha zilizotolewa na Rais Magufuli pamoja na mtumishi wa halmashauri zimetoka fungu gani?, wametoa mfukoni mwao au ni kodi za wananchi, wangetueleza ili tujue wazi kwa hivyo ni vita ya siasa tu inafanyika,”alisema Mbunda.
Mbunge wa Mikumi, Joseph Haule alisema Rais Magufuli anafahamu utaratibu wa sheria inayosimamia fedha hizo za majimbo, lakini alikuwa na lengo la kumharibia mbunge huyo aonekane hana msaada wowote kwa wananchi wake.
Alitoa mfano akisema katika jimbo lake mwaka 2015/16 alipokea Sh46 milioni ambazo aliwekeza kwenye kero ya mawadati. Licha ya kupunguza kero hiyo, alisema fedha hizo haziwezi kumaliza kero za wananchi katika kata 15 za jimbo lake.
“Fedha zinatolewa kwa kuangalia idadi ya watu na kiwango cha umaskini. Mwaka huu zimepunguzwa tena hadi Sh42milioni na kero bado ni nyingi. Kwa hivyo ni kweli Rais akiendesha siasa za namna hiyo inaweza kutuathiri kisiasa majimboni tukaonekana hatuna msaada wowote kwa wananchi. Lakini ni udhalilishaji ambao sitakubali utokee jimboni kwangu,” alisema Haule maarufu kama Profesa Jay.
Katika mkutano huo, Rais Magufuli alilazimika kuanzisha harambee ya ghafla huku akimtaka Ngombale kuchangia fedha hizo (Sh15 milioni) ambazo ni sehemu ya mfuko wa jimbo baada ya mkazi mmoja aliyepewa kipaza sauti kulalamika kuwa tatizo lao kubwa ni kituo cha afya.
Katika majibizano, mbunge huyo alisisitiza kutochangia kiasi hicho kwa kuwa tayari kamati ya mfuko wa jimbo ilishapanga bajeti katika kata zote 13, hivyo asingeweza kuweka ahadi asiyoweza kuitekeleza. Baada ya hapo Rais Magufuli aliamua kuchangia Sh20 milioni huku akimpiga kijembe mbunge huyo kwa wananchi.
Kutokana na mazingira hayo, Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa alisema fedha hizo ni kidogo na hivyo CCM kupitia Serikali yake inaweza kutumia mwanya huo kujitafutia uhalali wa kisiasa kupitia matatizo ya wananchi majimboni.
“Ni kweli itakuwa ‘threat’ kwetu upinzani endapo ataendelea kufanya siasa hizo chafu, Rais anatumia mbinu hiyo apendwe na wananchi ili baadaye wananchi waone upinzani hatuna lolote,”alisema.
Katibu Mkuu wa zamani NCCR-Mageuzi, Samweli Ruhuza, alisema Serikali ndiyo ina wajibu wa kujenga zahanati na huduma za kijamii na siyo mbunge, hivyo alichokifanya Rais Magufuli ni kutumia udhaifu wa wananchi wasioelewa wajibu wa Serikali.
“Kwanza kauli ile ameitoa kama mwenyekiti wa CCM na siyo Rais, kwa hivyo alikuwa anafanya siasa za kumkomoa mbunge, kuonyesha wabunge wa upinzani hawawezi kusaidia lolote siyo siasa nzuri hata kidogo,” alisema.
Hata hivyo, Mbunge wa Misungwi (CCM), Charles Kitwanga alimtetea Rais Magufuli na kusema mbunge huyo alikuwa na nafasi ya kutoa ahadi kwa wananachi hao, kwa kuwa awamu ya pili ya fedha hizo za mfuko hazijatoka bado.
Alisema kwa kuwa ni mwenyekiti wa kamati ya mfuko wa jimbo, angeweza kutoa ahadi na baadaye kuishawishi kamati hiyo kupeleka fedha hizo Somanga.
“Wabunge wote bado hatujapata awamu ya pili kwa hivyo ajilaumu mwenyewe kukosa ushawishi,”alisema.
Hata hivyo, Kitwanga alisema fedha za jimbo bado haziwezi kumaliza kero za wananchi kulingana na wingi wa changamoto.
fedha za mfuko wa jimbo
Kwa mujibu wa Sheria ya Mfuko wa kuchochea maendeleo ya jimbo (CDCF) namba 16 ya mwaka 2009, fedha hizo hutolewa na serikali kuu katika jimbo kwa viwango tofauti kutokana na vigezo mbalimbali ikiwamo idadi ya watu na kiwango cha umaskini ndani ya jimbo husika.
Madhumuni ya sheria hiyo ni kuhamasisha maendeleo katika majimbo kwa kugharamia utekelezaji wa miradi ambayo imeibuliwa na wananchi katika maeneo yao, lakini haikupata fedha katika Bajeti za Halmashauri.
Kwa mfano, fedha hizo hutumika kukamilisha ujenzi wa shule, kisima au barabara kwa matumizi ya wananchi katika eneo hilo. Aidha, fedha hizo hutolewa kila mwaka katika awamu moja au mbili na huingizwa moja kwa moja katika akaunti ya mfuko inayoratibiwa na Halmashauri.
Kabla ya matumizi ya fedha hizo kupangwa, mbunge wa jimbo husika anaweza kufanya ziara katika Kata akikutana na Baraza la Maendeleo ya Kata (BMK), ambao wanatoa vipaumbele vyao ili kujua ataanzia wapi kugawanya fedha hizo

No comments:
Write comments