WAZIRI Mkuu Mstaafu na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema), Fredrick Sumaye, amesema nchi inashindwa kuendelea
kwa sababu inaendeshwa kishabiki na kwamba mambo yanayofanyika hayana
maslai kwa taifa.
FREDRICK SUMAYE.
Akizungumza kwenye Kongamano la Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha)
na Umoja wa Vijana wa Vyuo Vikuu ambao ni wanachama wa Chadema (Chaso)
jijini Mbeya alipokuwa mgeni rasmi, Sumaye alisema mambo mengi yenye
masirahi ya taifa yakifanywa kimzaha yatasababisha madhara kwa taifa.
Sumaye ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Pwani, alisema
miongoni mwa mambo ambayo ni ya maslahi ya taifa lakini yanendeshwa
kishabiki ni mikataba ya madini na bajeti isiyokuwa na uhalisia.
Mengine aliyoyataja ni uendeshaji wa Bunge ambalo kikatiba ni chombo
huru ambacho hakipaswi kuiingiliwa na wabunge kufanya maamuzi kwa
maslahi ya vyama vyao vya siasa huku wengine wakishangilia na kuzomeana.
“Nchi kwa sasa inayumba na inashindwa kuendelea kutokana na kuendeshwa
kishabiki, Bajeti yetu ya mwaka uliopita fedha za miradi ya maendeleo
zilitolewa kwa asilimia 34 pekee na serikali ilikiri, lakini sasa hivi
wanakuja na bajeti kubwa zaidi ya hiyo ambayo haijatekelezwa na wabunge
wa CCM wanashangilia,” alisema Semaye na kuongeza:
“Mambo haya yanaliingiza taifa kwenye matatizo makubwa, deni la Taifa
linazidi kuongezeka, mikataba ya madini na mingine iliyokuwa ni yenye
maslahi ya taifa sasa inakuwa ni ya hasara kwetu, lakini ukiangalia
wabunge wanapiga meza wakishangilia.”
Sumaye alisema wasomi wa vyuo vikuu hawatumiki ipasavyo kwa maslahi ya
taifa ikiwamo kujadili mikataba na bajeti ya taifa na mawazo yao
kutumika katika kufanya marekebisho.
Alisema kipindi hiki ambacho bajeti ya 2017/18 inaanza kujadiliwa leo
bungeni, ilitakiwa midahalo mbalimbali ifanyike vyuoni kuichambua,
lakini kwa sasa ukifanya hivyo unaonekana umetumwa na vyama vya
upinzani, kitu ambacho siyo sahihi.
Alisema miaka ya nyuma viongozi wa serikali walikuwa wanahudhuria katika
Ukumbi wa Nkrumah katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kusikiliza mawazo
ya wasomi, lakini kwa sasa vyuo vikuu vinatumika kama sehemu ya vijana
kupata taaluma pekee.
Alisema Chadema imeamua kujitoa ili kupambana na taabu wanazopata wananchi kwa kuondoa ushabiki wa kisiasa.
No comments:
Write comments