Timu ya Yanga leo inatarajiwa kushuka uwanjani kuvaana na Tusker FC ya nchini Kenya kwenye michuano mipya ya SportPesa Super Cup, 2017 huku ikitarajia kushusha vifaa vipya vitatu.
Yanga
inatarajiwa kuvaana na Tusker majira ya saa 10:15 jioni kwenye Uwanja
wa Uhuru jijini Dar es Salaam huku mchezo wa kwanza ukitarajiwa kuanza
saa 8:00 mchana utakaowakutanisha Singida Utd na AFC Leopards.
Katika
michuano hiyo inashirikisha timu zilizodhaminiwa na SportPesa kutoka
hapa nchini Tanzania na Kenya, bingwa wake anatarajiwa kuvaana na Klabu
ya Everton ya Uingereza mwezi Julai, mwaka huu.
Meneja
Mkuu wa Yanga, Hafidh Saleh, alisema maandalizi yamekamilika na katika
mechi ya kesho wamepanga kuwatumia baadhi ya wachezaji wao wapya
waliojiunga na timu hiyo.
Saleh
alisema, miongoni mwa wachezaji wapya watakaokuwepo kwenye kikosi hicho
ni kiungo mshambuliaji wa zamani wa timu hiyo, Mrisho Ngassa, kiungo
mkabaji wa Kagera Sugar, Babu Ally Seif na beki mmoja wa pembeni wa Mbao
FC ambaye ni sapraizi.
"Kama
meneja nimewapokea wachezaji watatu wapya tutakaowatumia kesho (leo)
kwenye michuano ya SportPesa Super Cup akiwemo Ngassa na Seif na beki
mmoja wa pembeni wa Mbao.
"Pia
tutawatumia wachezaji wetu wengine wakongwe na vijana, kama unavyojua
nusu ya wachezaji wetu hawapo, wapo kwenye timu zao za taifa," alisema
Saleh.
Alipotafutwa
Ngassa mwenyewe ambaye alithibitisha hilo kwa kusema: Ni kweli nipo na
Yanga kwa ajili ya kujiandaa na michuano ya SportPesa, baada ya michuano
hiyo ndiyo nitajua nini kinaendelea, ingawa bado tupo kwenye
mazungumzo.”
No comments:
Write comments