Monday, 17 July 2017

TUNDU LISSU:LOWASA ATAPELEKWA MAHAKAMANI NA KUSHITAKIWA

Tundu Lissu: Nimepewa Siri Lowassa Atapelekwa Mahakamani na Kushitakiwa kwa Uchochezi

SeeBait
Wakati  Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, akiwa bado anakabiliwa na kesi kadhaa za uchochezi, amefytuka tena na kutoa maneno mazito juu ya viongozi wa Serikali, huku akisema kwa mujibu wa sheria za nchi, anaweza kukamatwa, lakini si kufungwa.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika Dar es Salaam jana, Lissu pia alisema amepata taarifa kutoka kwa mmoja wa askari polisi kuwa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, atafikishwa mahakamani wakati wowote kutokana na kauli alizozitoa juu ya  masheikh wa Uamsho. Hata hivyo, Mpekuzi haikuweza kujiridhisha juu ya usahihi wake.

Tundu Lissu ambaye baadhi ya kauli zake haziandikiki  kwa sababu za kimaadili, alisema pia watu ambao wanataka rais aongezewe muda wa kuongoza baada ya miaka 10 ya kikatiba, wabaki na kile alichokiita ni ujinga wao.

“Kuna watu wanaongea habari za kuongeza muda wa urais, tuwaambie tu huo wanaoleta ni ujinga, hivyo kaeni na ujinga wenu nyumbani kwenu,” alisema Lissu.

Akizungumzia taarifa za Lowassa kufikishwa mahakamani, alisema amezipata kutoka kwa mmoja wa maofisa wa ngazi za juu ndani ya Jeshi la Polisi.

Lissu alisema kuwa aliwasiliana na ofisa huyo jana asubuhi na kumtaka ajiandae kwa kesi hiyo ambayo ipo mbioni kupelekwa mahakamani.

“Nina taarifa nimeambiwa leo na lipolisi likubwa kabisa, maana hata wao hawafurahi sana, nimeambiwa jiandaeni mheshimiwa Lowassa atafikishwa mahakamani na kushtakiwa kwa uchochezi kwa sababu ya kuzungumzia uonevu wanaofanyiwa masheikh wa Uamsho,” alisema Lissu.

Alipoulizwa endapo kinga za kushtakiwa kwa viongozi, inawahusu pia mawaziri wakuu wastaafu, alisema kinga inamuhusu rais aliyepo madarakani pekee na mambo aliyofanya wakati akiwa Ikulu.

Hata hivyo, alisema kinga hiyo kwa marais, imechangia viongozi wengi wakiwa madarakani kufanya mambo mabaya.

“Kuna marais ambao ni wahalifu wakiwa marais, tunatakiwa tuwe na usawa ndani ya sheria, ikiwa muhalifu ukiwa Ikulu tukushughulikie au ukitoka tukushughulikie,” alisema Lissu huku akitolea mfano kwa Rais wa Brazil, Lula Da Silva.

Alisema Da Silva, sasa amehukumiwa kifungo cha miaka tisa baada ya kutoka madarakani kwa makosa ambayo aliyayafanya akiwa rais.

Alisisitiza kiongozi anapaswa kuwa na kinga kwa sababu ni msafi na si sababu ya uongozi wake.

Lowassa ambaye ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, alifika kwa mara ya kwanza polisi Juni 27, mwaka huu kwa wito wa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) na kuhojiwa kwa saa nne.

Aliripoti tena Makao Makuu ya Polisi Juni 29, Julai 13 na ametakiwa kuripoti Julai 20.

SOMA HAPA CHINI KUJIONEA MWENYEWE SIMBA INAVYOWADHIBITI WAPINZANI WAO NJE YA UWANJA
SIMBA WAJA KIVINGINE WAWAPIGA WAPINZANIWAO BAO LA KISIGINO NJE YA UWANJA KWA ISHU YA OKWI NA NIYONZIMA 

No comments:
Write comments