Kiungo mpya wa Simba, Haruna Niyonzima, ni kama ameupania mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga baada ya kusema kuwa wapinzani wao wanapaswa kujipanga vya kutosha kufuatia kuibuka na ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Gulioni FC kwani wameshamaliza kazi yao.
Juzi Jumamosi, Simba ilifanikiwa kuibuka na ushindi huo katika mchezo wake wa kirafiki dhidi ya Gulioni FC inayoshiriki Ligi Daraja la Pili Wilaya ya Mjini kisiwani hapa katika mchezo uliopigwa usiku kwenye Uwanja wa Amaan.
Mchezo huo ulikuwa ni wa mwisho kwa Simba kisiwani hapa kabla ya kurejea jijini Dar, tayari kwa mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga utakaopigwa keshokutwa Jumatano kwenye Uwanja wa Taifa, Dar.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Niyonzima alisema kuwa kwa upande wao tayari wameshamaliza kazi kutokana na matokeo ya ushindi huo ambapo amewataka wapinzani wao wajipange iwapo wanahitaji matokeo ya ushindi.
“Ushindi wa leo (juzi) kwetu una maana kubwa sana kwa sababu mchezo uliopita tulishindwa kupata matokeo na mchezo ulikuwa mgumu lakini tumejiuliza ndiyo maana tumefanikiwa kupata ushindi ambao unatoa picha halisi ya kambi yetu ilivyokuwa.
“Najua mchezo dhidi ya Yanga ambao nawajua vizuri hautakuwa rahisi kwangu kwa sababu utakuwa na presha kubwa kwa mashabiki wa timu yangu lakini wanapaswa kujiandaa kama wanataka kuibuka na ushindi, maana tayari sisi tumeshamaliza kile ambacho tumekilenga hapa na leo tumepata ushindi huu, naomba Mungu anijalie niweze kucheza vizuri siku hiyo,” alisema Niyonzima.
No comments:
Write comments