Saturday, 2 September 2017

KOCHA WA SIMBA OMOG AMSAKA AJIBU, KISA KIPO HAPA



BAADA ya hivi karibuni, mshambuliaji mpya wa Yanga, Ibrahim Ajibu kushindwa kuiongoza timu hiyo kuibuka na ushindi dhidi ya Lipuli FC katika mchezo wa Ligi Kuu Bara, kocha wake wa zamani Mcameroon, Joseph Omog ana neno juu ya mchezaji huyo. 

Omog ni kocha wa Simba, inafahamika kuwa timu yake hiyo na Yanga zina upinzani wa jadi, lakini hilo halijamzuia Omog kuamua kumshauri Ajibu kuhusu maisha yake ya soka. 

Kocha huyo wa zamani wa Azam FC, alikuwa bosi wa Ajibu msimu uliopita wakati alipokuwa Simba, ametoa neno hilo mara baada ya kumuona Ajibu akiitumikia Yanga hivi karibuni. Aliyeanza kuvujisha taarifa hizo ni mtu wa karibu wa kocha huyo ambaye aliliambia gazeti hili kuwa Omog amekuwa akitamani kukutana na Ajibu ili amwambie lile lililopo moyoni mwake baada ya kuona kiwango chake kikiwa 
ni cha kawaida. 


“Tangu Ajibu aende Yanga hawajawahi kuonana, alijaribu kumtafuta mara kadhaa kwa njia ya simu lakini hakumpata ila jambo kubwa analotaka kumwambia endapo atafanikiwa kuonana naye siku yoyote ni juu ya kubadili mfumo wake wa maisha kama kweli anataka kufanikiwa. 

“Unajua Omog alikuwa ni kama shabiki wa Ajibu, mara nyingi alikuwa hafurahishwi na jinsi alivyokuwa anaishi wakati alipokuwa Simba licha ya kutambua kuwa ana uwezo mkubwa wa kucheza soka, kwa hiyo hivi sasa anataka kumuona akiachana na maisha hayo na akili yake aweze kuilekeza zaidi mazoezini na kuzingatia yale yote anayoambiwa na viongozi wake wa ufundi,” alisema mtoa taarifa. Baada ya kupata taarifa hizo, Championi Ijumaa likampata Omog na kumuulizia juu ya taarifa hizo ambapo alisema: “Siyo kwamba nataka kumfuata Yanga ila nikipata bahati ya kukutana naye nitamshauri kuhusiana 
na hayo uliyoyasikia.

 “Ajibu ni mmoja kati ya wachezaji wachache hapa nchini wenye vipaji vya juu, hivyo siyo jambo zuri kumuacha akapotea, binafsi ni shabiki wake mkubwa na siku zote nimekuwa nikitaka kumuona anafika mbali na ikiwezekana awe kama Mbwana Samatta. “Ana kipaji cha hali ya juu, ni kitendo cha yeye sasa kubadilika na kutamani zaidi mafanikio.

” Ikumbukwe Ajibu alitua Yanga baada ya kuichezea Simba kwa misimu kadhaa tangu akiwa chipukizi, lakini tangu atue Yanga kwa dau la Sh milioni 70 bado hajaonyesha makali. Ajibu amekuwa akitajwa kama mchezaji asiyetilia maanani mazoezi, na wakati akiwa Simba mara kadhaa alikuwa akisusa kufanya mazoezi na kuchukulia vitu ‘simpo’ licha ya kuwa na kipaji kikubwa, hivyo kauli ya Omog kumtaka abadili mfumo wa maisha, huenda inalenga kumtaka aanze kuweka bidii katika kazi yake. Ajibu amekuwa akitajwa kama mchezaji ambaye anaweza kufika mbali kama akiweka akili yake yote katika soka.

CHANZO: CHAMPIONI

No comments:
Write comments